Habari
TANZANIA MWENYEJI MKUTANO WA 11 WA MERCK FOUNDATION 2024.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amebainisha kwamba, Mkutano wa 11 wa Taasisi ya Merck Foundation utafanyika Tanzania kwa mwaka 2024.
Akizungumza na washiriki zaidi ya 6000 wakati wa mkutano wa 10 wa Taasisi hiyo Mumbai nchini India, Oktoba 18, 2023 Waziri Dkt. Gwajima amewakaribisha nchini Tanzania na kueleza kuwa mbali ya kushiriki katika mkutano pia washiriki watapata fursa ya kutembelea vivutio mbalimbali vya utalii vilivyopo Tanzania.
Katika hotuba yake wakati wa Mkutano huo, Waziri Dkt. Gwajima amewasilisha taarifa ya ushirikiano wa Tanzania na Merck Foundation juu ya kuimarisha huduma za kijamii na Afya nchini hususan, mafunzo ya muda mfupi na mrefu kwa wataalam nchini hususani madaktari wa saratani na magonjwa ya kina mama na watoto.
Amebainisha kuwa, Taasisi ya Merck Foundation hadi sasa imetoa nafasi 42 za ufadhili wa masomo kwa madaktari kutoka Tanzania ambapo nafasi 15 ni kwa ajili ya mafunzo bobezi ya matibabu ya ugumba na afya ya kinamama na 29 kwa ajili ya mafunzo maalum ya kibingwa ya matibabu ya saratani, kisukari, Afya ya akili, huduma za matibabu ya dharura na magonjwa ya kuambukiza.
Amebainisha pia, Taasisi hiyo inamsomesha mshindi wa Dunia wa mashindano ya Mrembo mwenye ulemavu wa kusikia (Miss Deaf) kutoka Tanzania, Hadija Manyama, masomo ya Saikolojia katika Taasisi ya Ustawi wa Jamii.
Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza kwamba Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imepiga hatua kubwa ya uimarishaji huduma za Afya nchini hasa kwenye huduma za matibabu ya saratani kupitia huduma za kibingwa zinatolewa na hospitali ya Saratani ya Ocean Road.
Wakati wa mkutano huo wa 10, Waziri Dkt. Gwajima amepata fursa ya kushiriki katika majadiliano maalum yaliyolenga kuwainua wanawake kiuchumi, kijamii ambapo ameainisha mikakati inayofanywa Tanzania kuhusu makundi maalum wakiwemo wagumba.
Mkutano huu wa Taasisi ya Merck Foundation umewakutanisha watoa huduma za afya, watunga sera, wasomi, watafiti na vyombo vya habari vya afya ukifuatiliwa na zaidi ya watu 6000 kutoka nchi 70 zikiwemo Afrika, Asia na nchi nyingine duniani ambapo Wake wa Marais kutoka katika nchi za Angola, Botswana, Burundi, Cabo Verde, Afrika ya Kati, DR. Congo, Gambia, Ghana, Liberia, São Tomé and Príncipe, Namibia Malawi, Zambia na Zimbabwe wameshiriki na kutoa taarifa kuhusu ushirikiano na Taasisi ya Merck Foundation na nchi zao.
MWISHO