Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

RAIS SAMIA AWAPA TABASAMU WATOTO 286 IRINGA.

Imewekwa: 19 Jan, 2026
RAIS SAMIA AWAPA TABASAMU WATOTO 286 IRINGA.

Na Abdala Sifi WMJJWM– Iringa

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan amewapa tabasamu Watoto wenye mahitaji maalum 286 mkoani Iringa kwa kuwapa zawadi mbalimbali ikiwa ni kuwafanya washerekee sikukuu za mwisho wa mwaka kwa furaha na amani.

Hafla hiyo ya kugawa zawadi imefanyika tarehe 16 Januari 2025, katika vituo viwili vya Makao ya Watoto wenye mahitaji maalum ambavyo ni Mt. Felix Home Center wilayani Kilolo na Tosamaganga Home Center wilayani Iringa.

Akiwasilisha zawadi hizo kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, Afisa Ustawi wa Jamii Mkoa wa Iringa Ashery Mndalila amesema Serikali inawathamini watoto ambao ni hazina na nguvu kazi ya Taifa hivyo ni muhimu kuwajali na kuwapatia furaha, tumaini na upendo.

“Rais Samia anatambua na anasisitiza kuwa malezi ya mtoto ni wajibu wa pamoja, unaowahusisha wazazi, walezi na jamii ndio maana Serikali imeendelea kutekeleza Sera, Sheria na Miongozo mbalimbali ikiwemo Sheria ya Mtoto, inayolenga kulinda haki za Mtoto, kuhakikisha usalama wao, na kuboresha malezi, elimu, afya na ustawi wao bila ubaguzi”amesema Ashery.

Aidha ametoa wito kwa wazazi na walezi wote kuzingatia wajibu wao wa msingi kuhakikisha kwamba watoto wanapelekwa shule kwa wakati, wanahudhuria masomo kikamilifu na wanapata mahitaji ya msingi ya kielimu kwa kuwa elimu ni haki ya mtoto na msingi wa maendeleo ya Taifa.

Kwa upande wake Mlezi wa Watoto katika Kituo cha Mt.Felix Home Center Faustina Chota ameishukuru Serikali kwa kuendelea kutoa zawadi kwa watoto ambao wanalelewa katika makao hayo kwani inadhihirisha upendo na ushirikiano mzuri baina ya Serikali na Makao hayo huku akiahidi kuendeleza ushirikiano ili kuhakikisha watoto wenye mahitaji maalum wanapata mahitaji na haki zao za msingi.