Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

NAIBU WAZIRI MWANAIDI APONGEZA KAMATI YA MTAKUWWA KARATU

Imewekwa: 17 Mar, 2025
NAIBU WAZIRI MWANAIDI APONGEZA KAMATI YA MTAKUWWA KARATU

Na WMJJWM - Karatu- Arusha

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Mwananidi Ali Khamis, ameridhishwa na Maendeleo ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kwanza wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22)

Amesema hayo Machi 14, 2025 akiwa katika ziara Wilaya ya Karatu kwa lengo la ufuatiliaji na tathimini ya utekelezaji wa programu za malezi mbadala pamoja na programu ya uwezeshaji wa uchumi wa familia na vijana zinazotekelezwa na Shirika la SOS katika Mkoa wa Arusha.

Naibu Waziri Mwananidi amepongeza Kamati za MTAKUWWA katika ngazi zote kwa kuendelea kuwa waadilifu katika kusimamia na kutekeleza majukumu yenu kikamilifu na kuimarisha ulinzi wa mwanamke na mtoto.

"Endeleeni kuzingatia matakwa ya Mwongozo wa MTAKUWWA na kuanzisha kamati katika ngazi ya Wilaya, Kata na Mitaa kwa lengo la kupunguza aina zote za vitendo vya ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto" amesema Naibu Waziri Mwananidi.

Ameongeza kwamba Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kushirikiana Wizara za Kisekta inatekeleza Mpango Kazi wa Pili wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA II 2024/25 hadi 2028/29 kwa lengo kupunguza aina zote za ukatili kwa asilimia 50.

Akiyataja mafanikio ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Kwanza wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto (2017/18 – 2021/22) amesema Mpango huo umesaidia kuongezeka kwa huduma za mikopo yenye masharti nafuu kupitia mifuko tofauti. Mfano mikopo ya asilimia10 inayotokana na ya mapato ya ndani ya Halmashauri kutoka Shilingi Bilioni 15.6 mwaka 2017/28 hadi Shilingi Bilioni 35.6 mwaka 2021/22.

Mafanikio mengine ni kupungua kwa vitendo vya ukatili wa kingono kwa Wanawake kutoka asilimia 17 mwaka 2015 hadi asilimia 12 mwaka 2022, pamoja na kuongezeka kwa Vituo vya kulelea Watoto Wadogo mchana (ECD Centers) kutoka 1,103 hadi 2,649.

Aidha, Naibu Waziri Mwananidi amelipongeza Shirika la SOS kwa kuendelea kushirikiana na Serikali na kuwaomba viongozi wa Kamati hizo kutatua changamoto za kijamii.