MHE. MAHUNDI AONGOZA HATUA MPYA KUIMARISHA MSAADA KWA WANAFUNZI WENYE MAHITAJI MAALUM
Na WMJJWM Dar Es Salaam
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amezindua kamati maalum ya kuratibu na kuhamasisha michango kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi wenye mahitaji maalum.
Akizungumza baada ya kuzindua kamati hiyo Machi 11, 2026, Mkoani Dar Es salaam, Mahundi amesema uanzishwaji wa Kamati hiyo ni sehemu ya juhudi za serikali na wadau kuhakikisha wanafunzi wenye mahitaji maalum wanapata huduma na kuwa na mazingira bora ya kujifunzia na kuendeleza ndoto zao.
“Watoto wenye mahitaji maalum ni sehemu muhimu ya jamii yetu hivyo Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha wanapata fursa sawa za elimu, huduma na msaada unaowawezesha kufikia ndoto zao pia kamati hii itakuwa na jukumu la kuhamasisha jamii, taasisi na wadau mbalimbali kuchangia rasilimali zitakazosaidia kuboresha mahitaji ya wanafunzi hao ikiwemo vifaa vya kujifunzia, huduma za kijamii na mazingira rafiki ya elimu.,” amesema Mhe. Mahundi.
Naye Kaimu Katibu Tawala Mkoa wa Dar Es Salaam Lawrence Malangwa amesema ni muhimu ushirikiano wa jamii katika kuwasaidia watoto wenye uhitaji ili kuhakikisha hakuna mtoto anayekosa haki ya elimu kutokana na changamoto za maisha hiivyo tutasimamia vyema upatikananji wa vifaa na mtumizi kwa Watoto hao.
Kwa upande wake Mhazini wa Kamati ya Elimu Mama Tunu Pinda ameipongeza Wizara kwa kuendelea kuonesha dhamira ya dhati katika kutetea na kuimarisha ustawi wa makundi maalum nchini, akieleza kuwa hatua hiyo itachochea ari ya wadau wengi zaidi kujitokeza kusaidia wanafunzi wenye mahitaji.
Uzinduzi huo unatarajiwa kuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, wadau na jamii katika kuhakikisha wanafunzi wenye uhitaji wanapata msaada unaohitajika ili waweze kusoma na kufanikiwa kama watoto wengine.