Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YATAKIWA KUZINGATIA SHERIA NA MAADILI YA NCHI.

Imewekwa: 30 Jun, 2025
MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI YATAKIWA KUZINGATIA SHERIA NA MAADILI YA NCHI.

Na WMJJWM - Tabora

Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora, Ndg.Asanterabi Sang’enoi, ameongoza Mkutano wa mwaka wa Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Mhe. Paulo Chacha, uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mtemi Isike Mwanakiyungi.

Katika ufunguzi wa mkutano huo, Afisa Maendeleo ya Jamii Mkoa wa Tabora, Bi. Monica Yesaya, aliwapongeza wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO’s) kwa mchango wao mkubwa katika kusukuma gurudumu la maendeleo. Alisisitiza umuhimu wa mashirika hayo kuwasilisha kwa wakati taarifa za utekelezaji wa shughuli zao kila robo mwaka ili kuwezesha kufanyika kwa tathmini ya mchango wao katika jamii.

Kwa upande wake, Bi. Agneta John kutoka Shirika la JIDA, akizungumza kwa niaba ya NGO’s mkoa wa Tabora, alieleza changamoto zinazoathiri ufanisi wa mashirika hayo, zikiwemo gharama kubwa za uendeshaji, ukosefu wa fedha na rasilimali watu, pamoja na baadhi ya watumishi wa ofisi za umma kushindwa kutoa ushirikiano kwa mashirika hayo.

Vilevile alitoa ombi kwa serikali kuweka mazingira wezeshi ya upangishaji wa majengo ya serikali kwa bei nafuu, sambamba na kutoa maelekezo kwa watumishi wa umma kutoa ushirikiano kwa wadau wote wa maendeleo wanaofika katika ofisi za umma kupata huduma mbalimbali.

Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Ndugu Asanterabi Sang’enoi alieleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, imeendelea kuimarisha mazingira wezeshi kwa mashirika yote yanayotoa huduma kwa wananchi.

Alisisitiza umuhimu wa uwazi, uwajibikaji na ushirikiano baina ya mashirika na serikali, hasa katika kutekeleza shughuli za kijamii kama vile uchangiaji damu, usafi wa mazingira, upandaji miti, na kusaidia makundi maalum kama wagonjwa na watoto yatima.

“Sheria hairuhusu mashirika yasiyo ya kiserikali kujihusisha na siasa. Kwa yale yatakayopata vibali vya kutoa elimu ya mpiga kura, yahakikishe yanazingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo ya Tume Huru ya Uchaguzi,” alisema Sang’enoi.