MALEZI BORA NI MSINGI WA KUJENGA KIZAZI CHENYE MAADILI NA UZALENDO
Na WMJJWM – ARUSHA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Amon Mpanju, amefungua kikao kazi cha siku tano kinacholenga kuandaa jumbe mahsusi za kuelimisha wazazi na walezi kuhusu malezi bora ya watoto na ustawi wa familia katika jamii. Kikao hicho kinafanyika kuanzia Machi 9 hadi 13, 2026 jijini Arusha.
Kikao hicho kimewakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo watoto, wanafunzi, wakufunzi, waandishi wa habari, wasanii, wataalamu wa afya pamoja na wawakilishi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali ili kushirikiana kuandaa benki ya jumbe zitakazotumiwa kuelimisha jamii kupitia vyombo mbalimbali vya Habari.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Mpanju amewataka washiriki kubuni jumbe zenye nguvu zitakazosaidia kuleta mabadiliko chanya hasa kwa watoto na vijana wanaokabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo mmomonyoko wa maadili unaochangiwa na kuiga tamaduni za mataifa mengine kupitia maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano.
Mpanju amesisitiza kuwa malezi bora ni msingi wa kujenga kizazi chenye maadili na uzalendo, akionya kuwa jamii isiyoweka mkazo katika misingi ya malezi na makuzi ya watoto inaweza kuandaa Taifa lisilozingatia tunu muhimu kama utu, uadilifu, umoja na uwajibikaji.
Aidha, Mpanju ameeleza kuwa jitihada hizo zinaendana na malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050 ambayo inalenga kujenga rasilimali watu yenye tija kupitia elimu, ujuzi na ubunifu, hivyo kikao hicho ni sehemu ya utekelezaji wa dira hiyo ya muda mrefu ya maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake Meneja Miradi wa Shirika la DSW Tanzania Winnie Muine ameeleza kuwa wanaendelea kuboresha maisha ya vijana kwa kuwajengea uwezo kupitia utekelezaji wa afua za Afya ya uzazi, Stadi za maisha, kupinga ukatili wa kijinsia.
Ameongeza kwamba kupitia elimu wanayopata vijana watakuwa na ujasiri wa kufanya maamuzi sahihi kuhusu maisha yao, jambo litakalosaidia kujenga kizazi chenye afya, maadili na uwezo wa kukabiliana na changamoto za maisha.