MAHUNDI AWATAKA WAZAZI NA WALEZI KUWAJIBIKA KATIKA ULINZI WA WATOTO
Na Jackline Minja, WMJJWM
Dodoma
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka wazazi na walezi kutekeleza wajibu wao wa kuwalinda watoto dhidi ya vitendo vya ukatili na udhalilishaji, akisisitiza kuwa jukumu la malezi na ulinzi wa watoto linaanzia katika ngazi ya familia na siyo kusubiri Serikali iingilie kati baada ya mtoto kufanyiwa vitendo vinavyokiuka maadili ya jamii.
Mhe. Mahundi ametoa wito huo leo Novemba 2, 2026, jijini Dodoma, wakati akijibu maswali ya Wabunge kuhusu hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kutoa elimu kwa mabinti na jamii kuhusu kuripoti vitendo vya udhalilishaji.
“Wazazi na walezi wanapaswa kuwa karibu na watoto wao, kuwafuatilia, kuwapatia malezi bora na kuwaelekeza misingi ya maadili mema yanayozingatia mila, desturi na tamaduni za Kitanzania ili kuwakinga dhidi ya vitendo vinavyoweza kuhatarisha usalama na mustakabali wao” amesema Mahundi.
Ameongeza kwamba, Serikali inaendelea kutoa elimu kwa mabinti na jamii kupitia Mpango Kazi wa Kitaifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (MTAKUWWA), unaotekelezwa kupitia kamati za kisekta kuanzia ngazi ya Taifa hadi Vijiji na Mitaa.
Aidha amesema kila Kata ina Polisi Jamii wanaoshiriki kutoa elimu kwa wananchi, huku Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ikiratibu wadau wake, wakiwemo viongozi wa kimila na vyombo vya habari, katika kuelimisha jamii kuhusu namna ya kukabiliana na vitendo vya ukatili na udhalilishaji.
Amewataka Hivyo wananchi wanapaswa kuendelea kushirikiana na Serikali katika kutokomeza ukatili wa aina zote na kuhakikisha watoto wanakuwa katika mazingira salama yanayowawezesha kukua, kupata haki zao na kutimiza ndoto zao.
MWISHO