Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MAHUNDI AKAGUA MIRADI MLALE, ASISITIZA UZALENDO NA UTUNZAJI MIUNDOMBINU

Imewekwa: 26 Mar, 2026
MAHUNDI AKAGUA MIRADI MLALE, ASISITIZA UZALENDO NA UTUNZAJI MIUNDOMBINU

Na Jackline Minja, WMJJWM
RUVUMA
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Maryprisca Mahundi, ametoa rai ya kuimarishwa kwa uzalendo na utunzaji wa miundombinu ya chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale ili iweze kudumu na kunufaisha vizazi vya sasa na vijavyo.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mdahalo wa maadili na uzalendo uliofanyika chuoni hapo, Mahundi amesema kuwa ni jukumu la kila mwananchi kuhakikisha anailinda na kuitunza miundombinu ya umma, akisisitiza kuwa maadili na uzalendo ni msingi muhimu wa maendeleo ya Taifa.
“Uzalendo ni hali ya mtu kuipenda nchi yake, kulinda rasilimali za Taifa, kuwajibika na kufanya kazi kwa bidii kwa manufaa ya wote. Bila maadili thabiti, uzalendo wa kweli hauwezi kujengeka,” amesema Mahundi.
Aidha, amewataka vijana na jamii kwa ujumla kujiepusha na vitendo vinavyoharibu maadili na badala yake kuwa mstari wa mbele katika kulinda tunu za Taifa, huku akisisitiza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuboresha miundombinu ya taasisi za elimu ili kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Songea, Wilman Ndile, amesema mdahalo huo ni jukwaa muhimu litakalosaidia kujenga uelewa mpana wa masuala ya maadili na uzalendo kwa wanafunzi na wananchi.
Naye Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Mlale, Luciana Mvula , amesema chuo hicho kinaendelea kutekeleza programu za maendeleo ya ujuzi kwa wanafunzi kwa lengo la kuhakikisha kinazalisha wahitimu wenye uwezo wa kujiajiri na kuajirika, sambamba na kuchangia maendeleo ya jamii.