KATIBU MKUU MASWI ATAKA UTEKELEZAJI WA MRADI WA PAMOJA KWA MANUFAA YA WANANCHI
Na WMMJWM-Mwanza
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Eliakim Chacha Maswi, amewataka Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zinazotekeleza Mradi wa Kukuza Usawa wa Kijinsia Tanzania (PAMOJA) kuhakikisha utekelezaji wa Mradi huo unazingatia ubora, uendelevu na manufaa ya muda mrefu kwa wananchi.
Maswi ameyasema hayo tarehe 25 Septemba, 2026 jijini Mwanza wakati akifungua Kikao Kazi cha Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri zinazotekeleza Mradi wa PAMOJA unaotekelezwa katika mikoa 10 na Halmashauri 40, kilichofanyika katika Ukumbi wa Malaika Beach Resort.
Amesema mafanikio ya Mradi huo hayatategemea Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pekee, bali yanahitaji ushirikiano wa Ofisi ya Waziri Mkuu–TAMISEMI, Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa katika kupanga, kutenga maeneo, rasilimali, kusimamia utekelezaji, kutatua changamoto na kutoa taarifa kwa wakati.
Ameongeza kuwa Mradi wa PAMOJA ni uwekezaji wa Serikali unaolenga kubadili hali ya wanawake, watoto, familia na jamii kwa ujumla, ukiwa na maeneo mbalimbali ya utekelezaji, ikiwemo kuongeza fursa za kiuchumi kwa wanawake, kuimarisha juhudi za kuzuia na kukabiliana na ukatili wa kijinsia, kutoa huduma kwa manusura wa ukatili na kuwezesha upatikanaji wa huduma za malezi na maendeleo ya watoto wadogo kupitia vituo vya kijamii vya kulelea watoto wadogo mchana (CDCC).
Amehusisha utekelezaji wa Mradi huo na Ajenda ya Kitaifa ya Mageuzi ya Kijamii na Maendeleo ya Mtaji Watu katika Kufikia Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 (Jamii Ajenda – Dira 2050), ambayo Wizara inatekeleza kama nyenzo ya kufikia malengo ya Dira 2050, huku akiwataka viongozi hao kuangalia kwa mtazamo wa muda mrefu maeneo yanayotengwa kwa ajili ya miundombinu ya Mradi na kujiuliza kama maeneo hayo yataendelea kuwa na manufaa kwa jamii katika miaka 50 ijayo.