NA WMJJWM - ARUSHA
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii imeridhishwa na maendeleo ya mradi wa ujenzi wa jengo la utawala katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru (TCDI).
Hayo yamebainishwa katika kikao cha majumuisho kilichofanyika Machi 13, 2025, baada ya kamati hiyo kutembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jingo hilo na miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum.
Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mhe. Fatma Toufiq, ameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kusimamia kwa ufanisi miradi mbalimbali ya maendeleo, ikiwemo ujenzi wa jengo hilo la utawala. Pia, ametoa pongezi kwa uongozi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Tengeru, chini ya Mkuu wa Chuo hicho, Dkt. Bakari George, kwa usimamizi mzuri wa mradi huo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Tandahimba na mjumbe wa kamati hiyo, Mhe. Katani A. Katani, amesema kuwa serikali inahitaji wasimamizi wa miradi wazalendo kama wale waliopo kwenye mradi huo, kwani fedha zilizotumika zinalingana na maendeleo yaliyofikiwa.
Akisoma taarifa fupi ya mradi huo Bi. Janeth Zemba, Kaimu Mkuu wa Chuo hicho amesema kuwa hadi sasa mradi huo umefikia asilimia 70 ya utekelezaji na unatarajiwa Kukamilika ifikapo Mei 17, 2025 na hadi kukamilika utagharimu shilingi bilioni 5.664. Jengo hilo lenye ukubwa wa mita za mraba 894, lina ghorofa tatu na sakafu nne, likiwa na ofisi 44 na kumbi tano zenye uwezo wa kuchukua watu 545 kwa wakati mmoja.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mheshimiwa Mwanaid Ali Khamis, ameishukuru kamati hiyo kwa kuendelea kutoa mwongozo mzuri kuhusu usimamizi wa miradi na kutatua changamoto mbalimbali zinazojitokeza.
“Kwa niaba ya Wizara, tunapokea pongezi hizi kwa moyo wa shukrani. Tunawaomba msichoke kutuelekeza na kutusahihisha pale tunapokwenda kombo, ili kutimiza azma ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ya kuleta maendeleo kwa jamii,” alisema Mhe. Mwanaidi.