KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA USTAWI NA MAENDELEO YA JAMII YAJJADILI MTAKUWA II
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ustawi na Maendeleo ya Jamii, Dkt. Regina Malima, ameongoza kikao cha kamati hiyo kujadiili taarifa ya utekelezaji wa Mpango Kazi wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto Awamu ya Pili (MTAKUWWA II 2024/25–2028/29), ikijumuisha mafanikio, changamoto na mipango ya baadaye.
Akiwasilisha taarifa hiyo Oktoba 22, 2026 Bungeni jijini Dodoma, Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, ambaye amesema kuwa Serikali inaendelea kushirikiana na Wizara za kisekta pamoja na wadau mbalimbali katika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa MTAKUWWA II kwa lengo la kuhakikisha wanawake na watoto wanalindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na unyanyasaji.
Aidha, ameeleza kuwa utekelezaji wa mpango huo umeendelea kuonesha mafanikio, ikiwemo kupungua kwa vitendo vya ukatili wa kimwili na kingono dhidi ya wanawake, pamoja na kuimarika kwa uelewa wa jamii kuhusu umuhimu wa kutoa taarifa na kushiriki katika mapambano dhidi ya ukatili.
Baadhi ya Wabunge wameipongeza Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa kazi nzuri inayofanya katika kusimamia na kuratibu utekelezaji wa MTAKUWWA II, huku wakisisitiza umuhimu wa kuongeza nguvu katika kuhakikisha malengo mahususi ya ajenda hiyo yanafanyiwa kazi ipasavyo ili kupunguza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.
Wabunge hao wameeleza umuhimu wa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali, jamii na wadau mbalimbali katika kutekeleza mikakati ya kuzuia ukatili, kutoa taarifa za matukio ya ukatili na kuhakikisha hatua stahiki zinachukuliwa kwa wakati ili kujenga jamii salama kwa wanawake na watoto.