Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

ICGLR YAPONGEZA TANZANIA, UTEKELEZAJI AJENDA YA WANAWAKE, AMANI NA USALAMA

Imewekwa: 28 Oct, 2026
ICGLR YAPONGEZA TANZANIA, UTEKELEZAJI AJENDA YA WANAWAKE, AMANI NA USALAMA

Sekretarieti ya Jumuiya ya Nchi za Ukanda wa Maziwa Makuu (ICGLR), imeipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi zinazofanyika katika kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama kupitia Mpango wa Kitaifa wa Utekelezaji wa Ajenda hiyo wa mwaka 2025–2026.

Pongezi hizo zimetolewa wakati wa ziara ya kikazi ya ujumbe huo jijini Dodoma, iliyolenga kujifunza na kutathmini namna Tanzania inavyotekeleza ajenda hiyo, hususani katika kuimarisha ushiriki wa wanawake kwenye masuala ya amani na usalama.

Katika ziara hiyo, ujumbe umetembelea Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum ili kujionea mikakati ya kuratibu na kusimamia utekelezaji wa mpango huo nchini.

Akizungumza na ujumbe huo, Mkurugenzi wa Idara ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake, Yahaya Mmbaga, ameeleza mikakati ya wizara katika kutekeleza Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, akibainisha umuhimu wa kuwashirikisha wadau mbalimbali katika kujenga jamii yenye amani, usalama na mshikamano.

Kwa upande wake, kiongozi wa ujumbe huo, Dkt. Jean Kimonyo ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa hatua zinazochukuliwa katika kutekeleza sera hiyo na kueleza kuwa ujumbe huo utakuwa mabalozi wa kuhamasisha na kuitangaza mifano bora ya utekelezaji wa mpango huo katika ngazi ya kimataifa.

Amesema juhudi za wizara katika kuwajumuisha wadau mbalimbali wa jamii zinaonesha umuhimu wa ushirikishwaji katika kujenga jamii imara na yenye uwezo wa kudumisha amani na usalama.

“Hii ndiyo maana halisi ya jamii imara, kwani wizara hii mmewakusanya wana jamii wote kwa pamoja,” amesema.

Aidha, ujumbe huo unatarajiwa kutembelea madawati ya huduma za ustawi wa jamii katika Stendi ya mkoa wa Dodoma ya Nane Nane, Chuo Kikuu cha Dodoma na maeneo mengine ambako mpango huo unatekelezwa, kwa lengo la kujionea utekelezaji wake katika ngazi ya jamii.

Ziara hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha ushirikiano, kubadilishana uzoefu na kuendeleza utekelezaji wa Ajenda ya Wanawake, Amani na Usalama, inayolenga kuhakikisha wanawake wanashiriki kikamilifu katika kuzuia migogoro, kujenga amani na kuimarisha usalama katika jamii

slot gacor