MILA,DESTURI YA UKEKETAJI INAUA TUIACHE - WANANCHI MBULU
Jamii imeaswa kuhakikisha inawalinda watoto wa kike dhidi ya ukeketaji na kuachana na mila hiyo inayohatarisha maisha ya wasichana wengi.
Wito huo umetolewa na wananchi wa kata za Masqaroda, Hyderer na Gidhim katika Halmashauri ya wilaya ya Mbulu, mkoa wa Manyara Julai 23, 2026 wakati wa kampeni ya kusambaza Mkakati wa Kitaifa wa Kisekta wa Kutokomeza Ukeketaji ulioibua majadiliano ya namna ya kutokomeza ukeketaji wilayani Mbulu.
Wananchi hao wamesema ukeketaji kwa watoto wa kike umewaletea madhara wasichana na wanawake wengi kwa kutoka damu nyingi hasa wakati wa kujifungua na hata kusababisha vifo.
Mmoja wa wakazi wa kata ya Masqaroda Faustine Mbaha amesema wameelewa elimu iliyotolewa na wataalamu kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum pamoja na wadau wanaosambaza mkakati huo na atakuwa balozi wa kuelimisha wengine.
Naye mama Cesilia Gabriel Tarmo mkazi wa Masqaroda amewaasa wanawake kuacha vitendo hivyo kwani ni kinyume cha haki za binadamu na kinakosoa uumbaji.
Akizungumza katika kata ya Hayderer Mzee wa mila Gaudensi Naribaha amesisitiza kwamba ukeketaji unakemewa kwa sababu Serikali iko macho kufuatilia na kutoa miongozo na mikakati. Amewaasa wanawake waache vitendo hivyo kwani ndio mafundi wakubwa.
Kwa upande wake mama Yasinta Zakaria mkazi wa kata ya Hayderer, amesema ni vibaya kukeketa watoto wasichana.
“Sisi tuliokeketwa, tunajua madhara yake. Mila na desturi zinazoua sio nzuri” amesisitiza Yasinta.
Mkuu wa wilaya ya Mbulu Michael Semundu aloyeshuhudia mjadala huo wa wananchi amebainisha kuwa, Serikali imefanya jitihada kubwa ya kutokomeza ukeketaji hasa katika mkoa wa Manyara kutoka asilimia
70.8 mwaka 2010 hadi asilimia 43 mwaka huu 2026.
“Tunatambua bado kuna kazi kubwa,
Serikali ya mkoa haitavumilia vitendo hivyo hatua kali za kisheria zitachukiliwa kwa wahusika.
Wajibu wetu sote kuhakikisha watoto wa kike wanaishi salama, utu na haki za msingi.