DKT. GWAJIMA KWA MARA YA KWANZA NCHINI AZINDUA MWONGOZO WA URATIBU WA WAJANE, AHIMIZA USHIRIKI KATIKA FURSA ZA KIUCHUMI

Na WMJJWM – IRINGA
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, amezindua *Mwongozo wa Uratibu wa Wajane (2025)* katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wajane Duniani yaliyofanyika Iringa, Juni 23, 2025. Mwongozo huu unalenga kuboresha huduma za kijamii, kiuchumi na kisheria kwa wajane. Kwa mujibu wa Sensa ya 2022, Tanzania ina wajane zaidi ya milioni 1.3, huku Iringa ikiwa na zaidi ya 46,000.
Akitaja juhudi za Serikali chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Dkt. Gwajima amesema mikopo isiyo na riba inaendelea kutolewa kwa vikundi vya wanawake ili kuwawezesha kiuchumi. Pia, kupitia kampeni ya Mama Samia Legal Aid iliyoanza Aprili 2023, zaidi ya wananchi milioni 2.6 wamepata elimu na msaada wa kisheria kuhusu haki za ardhi, ndoa, wosia na ukatili wa kijinsia. Serikali imeanzisha Majukwaa 3,390 ya kuwawezesha wanawake – wakiwemo wajane – kushiriki kikamilifu katika maendeleo.
Dkt. Gwajima amewataka Wakuu wa Mikoa wote kusimamia utekelezaji wa mwongozo huu kwa kushirikiana na vyama vya wajane, ili kuwasaidia kushinda changamoto na kujikwamua kiuchumi, sambamba na kaulimbiu ya mwaka huu: *“Tuimarishe Fursa za Kiuchumi Kuchochea Maendeleo ya Wajane.”*
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilolo, Mhe. Edda Mdemu – akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Mhe. Peter Serukamba – amesema kuwa mkoa umejipanga kuendelea kutoa elimu kuhusu haki za wajane na kuimarisha ushirikiano na wadau wa maendeleo ili kuwafikia kwa ukaribu zaidi.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara, Bi. Felister Mdemu, amesema Serikali itaendelea kushirikiana na vyama vya wajane katika kutatua changamoto zinazowakabili. Ushirikiano huo utahakikisha wajane wanapata haki zao, kunufaika na fursa za maendeleo, na kuachana na mila kandamizi.
Akitoa taarifa ya Wiki ya Wajane, Afisa Maendeleo ya Jamii kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Bi. Saida Mgeni, amesema mafunzo yalitolewa kwa wajane 7,652 kutoka kata 57 kati ya 106. Mafunzo hayo yalihusu ujasiriamali, usimamizi wa mikopo, lishe bora, pamoja na haki za mirathi