AZEE NI TUNU, HAZINA YA HISTORIA YA TAIFA - KATIBU MKUU MASWI
Na WMJJWM – Dodoma
Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Eliakim Maswi amesema, Wazee ni tunu ya Taifa na hazina ya historia na nguzo muhimu ya maadili katika jamii, hivyo hekima na uzoefu wao vinapaswa kutunzwa, kuheshimiwa na kutumika katika kujenga jamii yenye amani, maadili na maendeleo endelevu.
Maswi ameyasema hayo Oktoba 01, 2026, Jijini Dodoma, katika kikao cha Baraza la Ushauri la Wazee Taifa ikiwa ni sehemu ya maandalizi ya maadhimisho ya Siku ya Wazee Duniani yaliyopangwa kufanyika kitaifa mkoani Songwe Novemba 5, 2026.
Amesema utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 unahitaji ushirikishwaji wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa ili kuhakikisha masuala ya wazee yanapewa nafasi katika mipango ya maendeleo ya nchi.
“Nipo tayari kusikiliza na kupokea maoni na changamoto za wazee nchini. Tukubaliane kufanya Baraza kuwa chombo chenye nguvu zaidi na kuweka msingi mpya wa uongozi katika utekelezaji wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050” amesema Maswi.
Amesisitiza pia umuhimu wa kuimarisha uratibu wa Mabaraza ya Wazee kuanzia ngazi ya Kata hadi Taifa, ili Baraza hilo kuwa chombo madhubuti cha ushauri na uwakilishi wa masuala yanayowahusu wazee na usimamizi wa maadili nchini
Aidha, amesema wazee wana wajibu wa kuwasaidia vijana kukabiliana na changamoto zinazowakabili, ikiwemo migogoro na mmomonyoko wa maadili, kwa kutumia uzoefu wao wa maisha na kuwa mfano mwema katika jamii.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Baraza la Ushauri la Wazee Taifa David Sendo ameipongeza Serikali kwa kuendelea kuwajali wazee na kuboresha huduma zinazowahusu, ikiwemo upatikanaji wa huduma za afya kupitia bima pamoja na matunzo kwa wazee.
Amesema Baraza la Ushauri la Wazee Taifa litaendelea kutekeleza wajibu wake wa kushiriki katika urejeshaji na uimarishaji wa maadili katika jamii, huku likikemea vitendo vinavyoweza kuathiri amani, umoja na utulivu wa Taifa.
Amesisitiza kuwa hekima ya wazee inapaswa kutumika kama daraja la kuunganisha vizazi, kutatua migogoro na kujenga jamii inayoheshimiana.
Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wazee yatakayofanyika Mkoani Songwe yanaongozwa na kaulimbiu inasema "Zama za Maisha Marefu, Tuboreshe Huduma kwa Wazee"..