Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

MAARIFA YA MAENDELEO YA JAMII YATUMIKE KUBORESHA MAISHA YA WANANCHI - NAIBU WAZIRI MAHUNDI

Imewekwa: 23 Jan, 2026
MAARIFA YA MAENDELEO YA JAMII YATUMIKE KUBORESHA MAISHA YA WANANCHI - NAIBU WAZIRI MAHUNDI

Na Jackline Minja MJJWM, Monduli- Arusha

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi, amewataka wanafunzi wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli kuzingatia kwa dhati malengo ya taaluma waliyoichagua na kuyatumia maarifa wanayojifunza chuoni katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.

Akizungumza na wanafunzi hao, Mhe. Mahundi amesema Serikali inahitaji wataalam wa Maendeleo ya Jamii wenye weledi, maadili na moyo wa kujitolea, nidhamu, uzalendo na uadilifu ambavyo ni misingi muhimu kwa wanafunzi ili waweze kuwa watumishi bora wa umma baada ya kuhitimu.

“Taaluma ya Maendeleo ya Jamii si ya darasani pekee, bali ni ya kwenda kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja kwa vitendo, kwa kutumia maarifa, maadili na ujuzi mnaoupata chuoni ili kushiriki kikamilifu katika kutatua changamoto za kijamii na kiuchumi katika jamii zetu,” amesema Mhe. Mahundi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli Boniface Daniel amesema, mafunzo yanayotolewa chuoni hapo yamejikita katika moduli kuu nne ambazo ni uhamasishaji na ushirikishwaji wa jamii, mipango na usimamizi wa miradi ya maendeleo, maendeleo ya kijamii na kiuchumi pamoja na uongozi, maadili na utawala bora katika jamii.

"Kupitia moduli hizo, chuo kinawaandaa wanafunzi kuwa na uwezo wa kufanya kazi kwa karibu na jamii, kubuni na kusimamia miradi ya maendeleo kwa ufanisi na kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo. Lengo letu ni kuhakikisha kila mhitimu anakuwa na ujuzi na mtazamo chanya unaomwezesha kuleta matokeo halisi katika jamii,” amesema Mkuu wa Chuo hicho.

Ziara hiyo ya Naibu Waziri Mahundi katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli imekuwa sehemu ya jitihada za Serikali katika kuimarisha elimu ya maendeleo ya jamii nchini, huku ikilenga kuhakikisha vyuo vinaendelea kuzalisha wataalam wenye ujuzi, maadili na uwezo wa kushirikiana na jamii katika kusukuma mbele ajenda ya maendeleo endelevu, kupunguza changamoto za kijamii na kuchochea ustawi wa wananchi kwa ujumla.

MWISHO