Usajili wa Vitambulisho vya Wafanyabiashara ndogondogo
- USAJILI WA VITAMBULISHO VYA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO
Zoezi la utambuzi na usajili wa wafanyabiashara ndogondogo utasimamiwa na Mratibu wa Dawati la wafanyabiashara ndogondogo katika Halmashauri husika kwa kushirikiana na Afisa TEHAMA wa Halmashauri husika, Maafisa Biashara na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika ngazi mbalimbali ikiwemo Kata, viongozi wa Serikali katika ngazi ya Msingi (Mtaa/Kijiji) pamoja na viongozi wa wafanyabiashara ndogondogo. Maafisa Biashara na Maafisa Maendeleo ya Jamii katika kila ngazi husika wana dhamana ya kuhakiki, kujiridhisha na kuthibitisha taarifa za anayesajiliwa kwenye mfumo kuwa, kweli ni mfanyabiashara ndogondogo aliyekusudiwa na Serikali kupatiwa kitambulisho hicho na si vinginevyo. Hivyo, endapo itatokea akasajiliwa mtu ambaye hausiki kwenye zoezi hili, Afisa aliyemhakiki na kumthibitisha atalazimika kuwajibika kwa nafasi yake kisheria.
Kwa msingi huo, mbali na uhakiki wa taarifa muhimu na kujiridhisha, ili mfanyabiashara ndogondogo aweze kutambuliwa na kusajiliwa kwenye mfumo huo atapaswa kuwa na sifa zifuatazo:-
i. Awe ni mkazi anayetambulika na uongozi wa Mtaa/Kijiji husika;
ii. Awe na barua ya utambulisho kutoka kwenye Serikali ya Mtaa/Kijiji;
iii. Awe na biashara halali inayotambulika na uongozi wa wafanyabiashara wa Mtaa/Kijiji wa eneo hilo;
iv. Awe na kitambulisho cha Taifa au Namba ya NIDA; na
v. Aweze kulipa gharama ya Ada ya usajili.