SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA PROGRAMU JUMUISHI YA MALEZI NA MAKUZI YA MTOTO.
Na WMJJWM Morogoro
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, amesema Serikali itaendelea kuimarisha Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha watoto wanapata malezi bora na huduma stahiki.
Wakili Mpanju ameyasema hayo Machi 16, 2026 mkoani Morogoro wakati wa ufunguzi wa kikao kazi cha siku mbili kinachowakutanisha wadau mbalimbali kujadili utekelezaji wa programu hiyo pamoja na namna ya kuendelea kuiboresha.
Amesema Serikali imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha lishe nchini ikiwemo kuandaa Mpango wa Taifa wa Kuimarisha Lishe wa mwaka 2021 hadi 2026, ambao umewezesha kuajiri maafisa lishe katika kila Halmashauri pamoja na kutoa elimu kwa jamii kuhusu umuhimu wa lishe bora hasa kwa wanawake wajawazito.
“Serikali imetekeleza mambo makubwa ikiwemo uandaaji wa Mpango huo ambao umetusaidia kuimarisha huduma za lishe nchini na kutoa elimu kwa wajawazito kuhusu umuhimu wa kula vyakula vyenye virutubisho ili kupambana na udumavu,” amesema Wakili Mpanju.
Aidha, amesema Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imejenga madarasa ya awali katika shule za msingi nchini ili kuimarisha malezi na makuzi ya watoto sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kupitia vyombo vya habari kuhusu maadili na ulinzi wa watoto.
Ameeleza kuwa programu hiyo inalenga kuhakikisha watoto wenye umri kuanzia miezi sifuri hadi miaka minane wanapata huduma muhimu zikiwemo afya, lishe bora, malezi yenye mwitikio, ujifunzaji wa awali pamoja na ulinzi dhidi ya vitendo vya ukatili.
Wakili Mpanju amesisitiza kwamba Taasisi za kiserikali,sekta binafsi, Taasisi za dini pamoja na wadau wa maendeleo kushirikiana kwa karibu ili kufanikisha tathmini ya utekelezaji wa programu hiyo na kuweka msingi wa kuandaa awamu ya pili ya Programu Jumuishi ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Mtoto nchini.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la TECDEN Mwajuma Kibwana amesema wataendelea kutekeleza afua za kuimarisha malezi ya awali ya mtoto ili kusaidi