WAZIRI GWAJIMA: WANAHABARI ANDIKENI ZAIDI KUHUSU MALEZI NA MAKUZI

Na MJJWM Dodoma.
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka waandishi wa habari kuongeza kasi ya kuandika habari za Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Watoto ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa Programu Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya 2021/22-2025/26).
Dkt. Gwajima amesema hayo leo Februari 28, 2025, jijini Dodoma wakati akizungumza waandishi wa habari Vinara wa Malezi na Makuzi ya Awali ya Watoto, Wamiliki wa Redio za Kijamii na Waratibu wa Klabu za Waandishi wa Habari kutoka Mikoa 26 ya Tanzania Bara.
Amesema waandishi wa habari wana wajibu wa kipekee kupitia kalamu taaluma zao, vyombo vya habari katika kuhamasisha jamii, kuchagiza uwajibikaji wa wadau wa watoto na kuhakikisha kuwa changamoto zilizopo zinajadiliwa na kupatiwa ufumbuzi.
“Tafiti zinaonesha kuwa redio ndio chombo cha habari kinachosikilizwa na idadi kubwa ya wanajamii. Hivyo, wamiliki wa redio na waandaji wa vipindi vya kueliemisha jamii, tumieni fursa hii ya mafunzo kuhakikisha kuwa mnaandaa vipindi vyenye ubora, pamoja na ushirikishwaji thabiti wa wadau na Serikali, ili maudhui ya vipindi yasaidie jamii kufanya maamuzi sahihii kuhusu malezi ya watoto”
Dkt. Gwajima ameongeza kwamba wanahabari wanatakiwa kuandika habari zinazohusu uanzishaji wa vituo vya kulelea watoto wadogo mchana kwenye jamii vikiwemo vile vinavyoanzishwa na kumilikiwa na jamii yenyewe kwa lengo la kutoa fursa kwa watoto kupata mwanzo mzuri wa malezi na kuwapa nafasi wazazi au walezi.
Amehitimisha kwa kusema kwamba Serikali inatendelea kushirkiana na wanahabari ili kufanikisha azma ya kuwafikia Wazazi au Walezi katika kuboresha huduma za malezi nchini, huku akiwaomba waandishi kuandika zaidi habari kuhusu ajenda hiyo kuelekea maadhimisho ya siku ya wanawake duniani, ikiwa kama sehemu ya kukumbusha umma kuhusu nafasi ya mwanamke kwenye malezi na makuzi ya watoto.