Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

TUTAENDELEA KUSIMAMIA KUIMARISHA JITIHADA USAWA WA KIJINSIA: WAKILI MPANJU

Imewekwa: 24 Feb, 2026
TUTAENDELEA KUSIMAMIA KUIMARISHA JITIHADA USAWA WA KIJINSIA: WAKILI MPANJU

Na Oscar Tarimo WMJWM Arusha

Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili  Amon Mpanju amesema Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya uongozi wa Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imeendelea kusimamia na kuimarisha jitihada kuhakikisha usawa wa kijinsia unazingatiwa kama msingi wa maendeleo endelevu kwa ustawi wa jamii na uchumi jumuishi.

Wakili Amon Mpanju ameyasema hayo wakati akifungua mafunzo ya uandaaji na uwasilishaji wa Habari zenye uchechemuzi wa masuala ya Jinsia tarehe 23, februari, 2026 jijini Arusha.

Wakili Mpanju amesema Serikali inaamini kuwa maendeleo ya kweli hayawezi kupatikana endapo sehemu ya jamii itaachwa bila kushiriki katika fursa zilizopo kwenye jamii ili kuondokana na mifumo ya ubaguzi na ukosefu wa haki unaotokana na jinsia.

Wakili Mpanju ameongeza kuwa usawa wa kijinsia siyo suala la wanawake pekee, bali ni ajenda ya kitaifa inayolenga kujenga jamii yenye haki, heshima, ushirikiano na maendeleo kwa wote hivyo mafunzo hayo yanasaidia kuleta uelewa kuwa usawa wa kijinsia hauondoi nafasi ya mwanaume katika jamii, bali kujenga jamii yenye uwiano, haki, na maendeleo kwa wote.

”Haya ni mafunzo ya kipekee na kimkakati kwa sababu yanawakutanisha waandishi wa habari ambao ni sauti ya jamii, Maafisa Maendeleo ya Jamii na Ustawi wa Jamii ambao ni nguzo ya ulinzi na ustawi wa watu, watendaji wa kata ambao ni kiungo cha Serikali na wananchi, pamoja na maafisa utumishi ambao wana jukumu la kusimamia mifumo ya ajira na usimamizi wa rasilimali watu kwa misingi ya haki na usawa.” amesema Wakili Mpanju

Amesitiza kuwa mafunzo hayo masuala ya usawa wa kijinsia yamekuja ikiwa ni utekelezaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inayosisitiza kuwepo na usawa kwa watu wote pamoja na Mikataba mbalimbali ya Kimataifa iliyokubakiwa nchini ambayo inayosisitiza uwepo wa usawa wa kijinsia.

“Tunapopinga ubaguzi wa kijinsia, tunalenga kuondoa mifumo inayomnyima mwanamke au mwanaume fursa kwa misingi ya jinsia. Kwa hiyo, jumbe zetu lazima ziwe jumuishi na zielekeze jamii kwenye mshikamano, ushirikiano, na maendeleo ya pamoja.” amesisitiza Wakili Mpanju

Wakili Mpanju amesisitiza kuwa jumbe zitakazoandaliwa na kusambazwa zina nafasi kubwa ya kujenga na kusaidia kuimarisha mshikamano wa familia na jamii,  na kuwaomba washiriki kuzingatia maadili Ili kufikia lengo lililokusudiwa badala ya kupotosha jamii.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini Raymond Mushumbusi amesema Mafunzo hayo yamegawanyika katika Kanda tano ambazo zitakutanisha washiriki kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania Bara wakiwemo Maafisa Maendeleo ya Jamaii, Maafisa Ustawi wa Jamii, Maafisa Tawala, watendaji wa Kata, Maafisa Habari na waandishi wa Habari kutoka katika Radio za kijamii.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu TAMISEMI Petro Mbwanji amesema wao kama watekelezaji wa mafunzo hayo wapo tayari kusimamia utekelezaji wa mafunzo hayo hasa katika kutumia jumbe husika katika kutoa elimu kwa wananchi kupitia njia mbalimbali katika ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa.