WAZIRI GWAJIMA: TUSHIRIKIANE KUIMARISHA HAKI NA USAWA WA KIUCHUMI KUPITIA PROGRAMU YA KIZAZI CHENYE USAWA (GEF)

WAZIRI GWAJIMA: TUSHIRIKIANE KUIMARISHA HAKI NA USAWA WA KIUCHUMI KUPITIA PROGRAMU YA KIZAZI CHENYE USAWA (GEF)
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa wadau wote kushirikiana kwa dhati ili kuhakikisha mafanikio ya Programu ya Kizazi Chenye Usawa (GEF) yanakuwa endelevu.
Akizungumza katika kikao kazi cha kuwasilisha na kupitia taarifa za utekelezaji wa programu hiyo Februari 14, 2025 jijini Dodoma, Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa kuwa na mikakati thabiti na ushirikiano wa pamoja katika kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii.
Katika hotuba yake, Waziri Dkt. Gwajima meeleza kwamba Programu ya Kizazi Chenye Usawa imejikita katika kuhakikisha fursa sawa zinatolewa kwa wanawake, wanaume, vijana na makundi maalum, ili kujenga jamii yenye usawa wa kijinsia.
"Usawa wa kijinsia siyo tu suala la haki za binadamu, bali ni kichocheo kikuu cha maendeleo endelevu ya taifa letu," amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Aidha, Waziri Dkt. Gwajima amebainisha kuwa Serikali imeweka mipango madhubuti kuhakikisha kuwa malengo ya GEF yanafikiwa, ikiwemo kuimarisha sera na mifumo inayowezesha ushiriki wa makundi yote kwenye shughuli za kiuchumi, kijamii na maendeleo kwa ujumla.
"Tunahitaji kushirikiana kama wadau wa maendeleo ili kuhakikisha tunawajengea vijana wetu mazingira salama na yenye fursa sawa. Hii ni muhimu kwa sababu kizazi cha leo ndicho kitakachojenga Tanzania ya kesho," amesisitiza.
Waziri Dkt. Gwajima amesisitiza kuwa ni muhimu kwa wadau wote ikiwemo Wizara, Taasisi na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, kuhakikisha taarifa za utekelezaji wa afua hizi zinakusanywa, kuchakatwa na kuwasilishwa kwa wakati ili kufanikisha malengo ya programu husika.