Habari

Imewekwa: Jan, 07 2023

​WAZIRI GWAJIMA APONGEZA MIRADI YA BIL 1 CHUO CHA MAENDELEO YA JAMII MONDULI

News Images

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum amepongeza hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Miradi ya Maendeleo katika Chuo cha Maendeleo ya Jamii Monduli Mkoani Arusha.

Akikagua Miradi hiyo chuoni hapo ambayo imegharimu jumla ya sh. bilioni 1, Januari 06, 2023 Waziri Gwajima amekipongeza Chuo hicho kwa usimamizi mzuri na kuhakikisha Miradi inakwisha kwa wakati na baadhi yake kuanza kutumika

Miradi hiyo ni pamoja na darasa la kompyuta na ofisi, ukumbi mpya wa mihadhara unaochukua wanafunzi 450 na ukumbi pacha za mihadhara zinazochukua wanafunzi 350 kila mmoja.

Hata hivyo Waziri Gwajima amevitaka Vyuo vya Maendeleo ya Jamii nchini kuwa mstari wa mbele katika kufanikisha ajenda za maendeleo kwenye jamii kwani vyuo hivyo vina nafasi kubwa ya kubadili fikra za wananchi katika masuala mbalimbali na kutatua changamoto zilizopo ikiwemo ukatili wa kijinsia na kwa watoto ikiwemo wale wanaoishi mitaani na wanaopata mimba za utotoni.

"Dhana ya ushirikishwaji wa wananchi ni muhimu katika kutatua changamoto zilizopo kwenye jamii ndiyo sababu, Wizara iliamua kuzianzisha ili iwe mbinu ya kufikia Maendeleo hivyo vyuo hivi vina mchango mkubwa eneo hili" amesema Waziri Gwajima.

Aidha, Waziri Gwajima ametoa wito kwa wahitimu wote katika fani ya uanagenzi wafuatiliwe na kuunganishwa na fursa za mikopo zilizopo ili watumie taaluma hiyo kuisaidiia Jamii kwa kujiajiri na kuajiri wengine.

Akiwasilisha taarifa ya miradi Mkuu wa Chuo hicho Boniphace Benedict amesema Chuo kicho kimejenga Miradi hiyo kwa Fedha za Serikali kuu kupitia Wizarani.

Mkuu huyo wa Chuo ameomba kutatuliwa Kwa changamoto ya Hosteli za wanafunzi kwani udahili umeongezeka ambapo mpango ni kujenga hosteli itakayochukua wanafunzi 600.

Awali mwakilishi wa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha Rose alisema, Jiji hilo linatarajia kutoa mikopo yenye thamani ya shilingi milioni 200 kwa vikundi vya Wanawake, vijana na watu wenye Ulemavu kutokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani Kwa kipindi cha mwaka 2022/23.

"Uwezeshaji wananchi kiuchumi kutokana na asilimia 10 ni shirikishi kuanzia ngazi ya kata hadi Wilaya na Kamati ya fedha imeshapitishwa, tunatumia mfumo wa sasa" amesema Rose na kuongeza fursa za mikopo mingine kuwa ni mfuko wa vijana, mfuko wa Wanawake na mfuko wa Tarura.

Kwa upande wake mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Arusha Tateni Malack amesema Chuo hicho ni msaada mkubwa Jamii ya Arusha na kuomba Wizara itatue changamoto ya hosteli kwani wanafunzi ni wengi.

MWISHO