WAZIRI DKT. GWAJIMA ANAFANYA KAZI KUBWA SANA - DKT. BITEKO

Na WMJJWM, Dodoma
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati Mhe. Doto Mashaka Biteko (Mb), amempongeza kwa dhati Waziri wa Maendeleo ya Jamiii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima @gwajimad kwa uongozi wake mahiri katika kuisimamia wizara yake kwa ufanisi.
Amempongeza Waziri Dkt. Gwajima kwa uwezo wake wa kutatua changamoto mbalimbali za wananchi Saa 24 kwa siku bila kuchoka na kuimudu vyema Wizara yake pamoja na ujasiri wake wa kutoa majibu sahihi na ya wakati kupitia mitandao ya kijamii.
Naibu Waziri Mkuu Dkt. Biteko ameyasema hayo wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii Tanzania (CODEPATA) Mei 07, 2025.
Aidha Dkt. Biteko ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inautambua mchango mkubwa wa taaluma ya Maendeleo ya Jamii hivyo ametoa wito kwa Taasisi zote kuwashirikisha wataalam wa Maendeleo katika mipango yote ya Maendeleo kuanzia awali.
“Naomba muendelee na jukumu lenu la kuwahamasisha wananchi kutambua na kuchangamkia fursa zilizomo kwenye jamii ikiwemo mikopo inayotolewa ili kuweza kuwainua kiuchumi na kuletea maendeleo katika jamii” alisisitiza Dkt. Biteko.
Kwa upande wake Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima awali akimkaribisha mgeni rasmi amewataka wataalam hao wa Maendeleo ya Jamii kuwa mabalozi wazuri wa shughuli za Maendeleo zilizofanywa na Serikali ya awamu ya sita kwa wananchi wakati nchi inaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
"Ninyi ni mainjinia wa mafanikio ya Jamii, nawapongeza sana kwa kuitumia taaluma yenu kuwa chachu ya kuleta maendeleo katika nchi yetu, mkawe mashahidi wazuri kwa wananchi tunapoenda kwenye uchaguzi mwezi Oktoba" ameeleza Waziri Dkt. Gwajima
Naye rais wa Chama cha Wataalam wa Maendeleo ya Jamii (CODEPATA) Victor Kabuje akitoa salam za Chama hicho ameishukuru Serikali kwa kuajiri Wataalam wa Maendeleo ambao wamekuwa chachu ya kurahisisha uwajibikaji na kuwafikia wananchi kuanzia ngazi ya Kata.