Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WAZIRI DKT. GWAJIMA AWATAKA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA.

Imewekwa: 09 May, 2025
WAZIRI DKT. GWAJIMA AWATAKA WAZAZI KUZINGATIA MALEZI BORA.

Na WMJJWM, Dodoma.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewataka wazazi nchini kuzingatia malezi na makuzi bora ya watoto tangu kipindi cha mimba hadi mtoto anapofikisha umri wa miaka 18.

Dkt. Gwajima amesema hayo Mei 08, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuelekea Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Familia itakayofanyika Mei 15, 2025. 

Waziri Dkt. Gwajima amesema majukumu ya familia ni mengi lakini kubwa ni kutoa huduma ili kukidhi mahitaji ya watoto na familia sambamba na kusimamia malezi na makuzi mema ya watoto. Aidha, amesema familia ina jukumu la kurithisha mila na tamaduni nzuri kwa watoto na familia kwa ujumla kizazi hadi kizazi.

Ameongeza kwamba Taifa lolote lenye maendeleo endelevu ya kiuchumi, kisiasa na kijamii hutokana na namna ambavyo watoto wamelelewa na kukuzwa kwa kuzingatia misingi ya malezi chanya inayoendana na maadili, mila na desturi njema za kitanzania.

Waziri Dkt. Gwajima amewahimiza Wazazi na Walezi kutimiza wajibu wao wa malezi na matunzo ya watoto ili kumkuza mtoto kuwa na tija kwa familia na taifa kwa ujumla ili kufanikisha hilo amewaomba wazazi kutenga muda wa kuzungumza na watoto wao mara kwa mara ili kuimarisha muunganiko (bond) baina ya mzazi na mtoto hasa kwa kuwekeza nguvu nyingi zaidi za malezi kwenye umri wa chini ya miaka 8 kipindi ambapo, ubongo unakua kwa asilimia 90.

Pia amewataka wazazi na walezi  kujua maendeleo ya mtoto na changamoto zinazomkabili kwa wakati na kuzipatia ufumbuzi kabla hazijaleta madhara makubwa. 

Akieleza jitihada za Serikali kupitia Wizara anayoisimamia  kuwa inaendelea kuimarisha mifumo ya kisheria kwa kufanya marekebisho ya Sheria Tatu ambazo ni Sheria ya Mtoto, Sura ya 13, Sheria ya Makosa ya Kimtandao, Sura ya 443, na Sheria ya Msaada wa Kisheria, Sura ya 21 huku marekebisho hayo yakilenga kuondoa upungufu unaojitokeza katika utekelezaji wa masharti katika sheria husika ili kuimarisha ulinzi na maslahi bora ya mtoto.

Katika kuimarisha mahusiano baina ya wenza na watoto katika familia Waziri Dkt. Gwajima amewasihi Wenza kutenga muda wa kutoka na familia yaani "outing" kwa lengo la kutafakari na kufurahia maisha ya mahusiano lakini pia kupata nafasi ya kujadili na kumaliza tofauti zao. 

Maadhimisho ya mwaka huu, yatafanyika katika Mikoa na Halmashauri zote nchini ambapo zimetakiwa kuimarisha afua za kuelimisha na kuchochea mijadala katika jamii kwa kutumia wataalam wa malezi chanya ya watoto na familia ikiwa pamoja na viongozi wa Dini ili kutafuta ufumbuzi wa migogoro katika familia na malezi duni ya watoto. 


Madhimisho ya mwaka huu yanaongozwa na Kauli mbiu isemayo “Mtoto ni Malezi; Msingi wa Familia Bora kwa Taifa Imara’’. Ikilenga kutathmini nafasi ya familia katika ustawi na maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla.