WAZIRI GWAJIMA AKUTANA NA RC MAKONDA, APONGEZA MAANDALIZI YA KILELE CHA SIKU YA WANAWAKE DUNIANI 2025

Na. WMJJWM -Arusha
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amepongeza kamati za maandalizi kwa kazi nzuri wanayoendelea kuifanya kuelekea Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani tarehe 8 Machi 2025 huku Arusha ikiwa mwenyeji wa kilele hiki kitaifa.
Dkt. Gwajima ameeleza hayo alipokutana na kamati za maandalizi ya kilele hicho Februari 25, 2025 Jijini Arusha yakayofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid, yakiongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
“Ninapongeza Kamati ya Maandalizi kitaifa chini ya Uongozi wa Bi. Sarah Masasi pamoja na Kamati zote katika ngazi ya Mkoa kwa kazi kubwa na nzuri inayofanyika kuhakikisha maadhimisho haya yanakuwa ya mafanikio. Hii ni siku muhimu kwa wanawake wa Tanzania na tunapaswa kuhakikisha inadhimishwa kwa heshima, hamasa na mafanikio makubwa. amesema Waziri Dkt. Gwajima
Dkt. Gwajima amesema, maandalizi hayo yanajumuisha matukio muhimu kama uzinduzi wa maadhimisho tarehe 1 Machi 2025, Makongamano saba ya Kikanda yenye ajenda mbalimbali za Wanawake na Maendeleo.
Pamoja na pongezi kwa kamati za maandalizi, Waziri Gwajima amempongeza na kutoa shukrani kwa Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. Paul Makonda kwa usimamizi mzuri wa maandalizi, akisema juhudi zake zimewezesha maandalizi kufanyika kwa ufanisi mkubwa huku akiwahimiza Wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki katika sherehe hizi muhimu kwa maendeleo ya wanawake nchini.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mhe. Paul Makonda amesema maandalizi yataendelea kwa nguvu mpya ili kuongeza hamasa na kuhakikisha siku hiyo inakuwa ya kipekee kwa wanawake na wananchi wote watakaoshiriki.
Aidha baadhi ya wakuu wa kamati za maandalizi ya siku hiyo wamesema kuwa, juhudi zinaendelea vizuri kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika vizuri na kuhakikisha kila mmoja anajivunia kushiriki.