Habari

Imewekwa: Nov, 01 2023

​WAZIRI GWAJIMA AKAGUA FUKWE NA VITUO VYA MASAJI KUBAINI VICHOCHEO VYA MMOMONYOKO WA MAADIL

News Images

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amewaomba viongozi wa Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa zenye fukwe nchini kuhakikisha wanafuatilia na kubaini mianya ya kuchochea mmomonyoko wa maadili na ukatili wa kijinsia na kuchukua hatua haraka.

Mhe. Gwajima ametoa ombi hilo Oktoba 30, 2023, akizungumza na waandishi wa Habari mara baada ya ziara ya siku mbili mkoani Dar-es- Salaam iliyokuwa na lengo la kufuatilia huduma za ufukweni na saluni hususan wachuaji (massage) ambapo hivi karibuni baadhi yao wametuhumiwa kuhusika na vitendo vya kuchochea mmomonyoko wa maadili na ukatili wa kijinsia.

Amewaomba wananchi wote kuendelea kuibua matendo maovu ambayo ni kinyume na maadili kwani Serikali itafanikiwa iwapo jamii itatoa ushirikiano.

"Viongozi na watumishi wa Umma muwape ushirikiano wananchi wanaotoa taarifa na kuibua masuala yaliyo kinyume na maadili kwa kuchukua hatua au kufanyia kazi sio hadi viongozi wa juu wanyanyuke. Nikiona kimya ndio maana nanyanyuka, tukishikana na wananchi watatuamini," amesema Waziri Dkt. Gwajima.

Akieleza kilichofanyika wakati wa ziara hiyo Waziri Dkt. Gwajima amesema, amefanikiwa kuzungumza na watoa huduma ya kufundisha kuogelea maarufu kama 'Beach Boys', wahusika wameeleza kuwa hawahusiki na vitendo vya ukatili kwani wao wanatambulika kisheria kuanzia ngazi ya mtaa. Aidha, wamesema ukatili unafanyika miongoni mwa watu wanaokwenda kama waogeleaji wakiwa na wapenzi wao ambapo nao husikia tu kwenye vyombo vya Habari.

Kutokana na hali hiyo, Waziri Gwajima amebainisha kwamba kuna kila sababu ya kuwa na mwongozo wa ushirikiano kati ya Serikali na vikundi hivyo ili kuboresha huduma na taratibu husika zijulikane na jamii inayokwenda kuogelea maeneo hayo.

Aidha, ameelekeza mafunzo ya uongozi kwa vikundi hivyo yafanyike ili vijiendeshe wenyewe kwa ubora zaidi na usalama kwa wateja pamoja na kujengewa uwezo wa kuimarisha matangazo ya huduma zao, kupima afya, mawasiliano na wateja na kuwa na bima za maisha na afya.

Ameongeza pia vikundi hivyo vinapaswa kuunganishwa na Kamati za Mpango wa Taifa wa Kutokomeza Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto yaani MTAKUWWA ili kuongeza nguvu katika kukabiliana na vitendo ukatili.

Kwa upande wa Huduma za uchuaji (massage) Waziri Dkt. Gwajima amewataka wamiliki kuhakikisha wanafuata sheria na taratibu na kutofanya mambo yasiyoruhusiwa kinyume na leseni walizopewa na Mamlaka.

Wakati huo huo Waziri Dkt. Gwajima amepokea Taarifa ya Mkoa wa Dar-es-Salaam na Wilaya ya Kinondoni kuhusu matukio yaliyochukuliwa hatua ikiwemo kuifungia moja ya saluni kwa kukiuka masharti ya leseni na kuchochea mmomonyoko wa maadili pamoja na kuimarisha vikundi vinavyosaidia watu kuogelea.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni Mhe. Saadi Mtambule amewaonya watoa huduma ambao wanakwenda kinyume na taratibu za huduma hizo kwa kuchochea mmomonyoko wa maadili wilayani humo na kuahidi kuendelea kuwafuatilia na kuwachukulia hatua kali.

Naye mmoja wa watoa huduma za kuogelea Musa Myamba ameiomba Serikali kuwasaidia kuboresha maeneo yao ili waogeleaji wawe salama muda wote na kwamba wao wakiwa waokozi watahakikisha masuala ya uvunjaji wa maadili hayatokei.