MAHUNDI AHIMIZA WAHITIMU MAENDELEO YA JAMII KUTATUA CHANGAMOTO ZA JAMII
Na WMJJWM- Mbeya
Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhandisi Maryprisca Mahundi, ameagiza Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole kupitia dhana ya ushirikishwaji jamii kutatua changamoto za jamii ikiwemo kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia na kutaka kazi hiyo kuwa endelevu ndani na nje ya Chuo.
Mahundi amezungumza hayo wakati wa mahafali ya kumi na sita ya chuo cha maendeleo ya jamii CDTI uyole yaliofanyika viwanja vya michezo Chuo cha Maendeleo ya Jamii Uyole na kusema licha ya siku kumi na sita za kupinga ukatili kufanyika lazima zoezi hilo likawe endelevu
Ameitaka jamii inayozunguka Chuo na kila mwanafunzi kuwa mjumbe kupeleka elimu ya kupinga ukatili hasa wanaporudi nyumbani au katika sehemu za kazi.
Mahundi amesema ni mategemeo ya Wizara na Serikali kwa ujumla kuwa watumishi na wanafunzi wa Chuo hicho wataendelea kutimiza wajibu kwa kufanya kazi kwa bidii na kuendelea kuzingatia sheria, taratibu, kanuni na miongozo mbalimbali ya Kitaifa na kama wakifanya hivyo wataendelea kutoa wahitimu mahiri na wenye maadili mema wanaoweza kushindana katika soko la ajira .
Kwa upande wake Mkurugenzi anayesimamia Vyuo vya Maendeleo ya jamii nchi kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Neema Ndoboka amesema Vyuo vya Maendeleo ya jamii nchini vimekuwa na mchango mkubwa katika kuleta maendeleo.
Awali akisoma taarifa ya Chuo hicho Makamu Mkuu wa Chuo anaeshughulikia Taaluma Spay Mwangomile amesema kwa ujumla nidhamu ya wanafunzi imekuwa ya kuridhisha uku wakifundishwa maadili mema,uadilifu na uwajibikaji popote watakapokuwa wakiwa kama mabalozi wa Chuo hicho na kuwataka wanafunzi waliohitimu chuo hicho kuwa wabunifu
Jumla ya wahitimu 530 wakiwemo wanawake 272 na wanaume na 258 wamehitimu katika mahafali ya Chuo hicho katika ngazi ya Astashahada na Shahada