WAZIRI GWAJIMA AAGIZA WIZARA KUENDELEZA AGENDA YA RAIS SAMIA KUPANDA MITI
📌 AAGIZA TAASISI ZILIZO CHINI YA WIZARA KUENDELEZA AGENDA HIYO.
📌 MAKUNDI YA WATOTO, WAZEE, WAJANE, WANAWAKE, WANAUME NA WAFANYABIASHARA NDOGONDOGO KUHUSISHWA
*Na Said Said WMJJWM Dodoma*
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ameagiza Wizara na Taasisi zake kuweka mikakati ya kuendeleza agenda ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya utunzaji wa mazingira kwa kuendelea kupanda Miti katika Taasisi zilizopo chini ya Wizara.
Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo tarehe 27 Januari, 2026 katika zoezi la upandaji Miti kwa lengo la kumuunga mkono Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa uamuzi wake wa kuadhimisha siku yake ya kuzaliwa kwa vitendo vya kupanda miti ili kulinda mazingira.
Waziri Dkt. Gwajima amesema, suala la utunzaji wa mazingira kupitia upandaji Miti linatakiwa kurithishwa kwenye vizazi hivyo, hatuna budi Wizara hii kupitia programu za malezi na makuzi na kupitia makundi mbalimbali tunayoyasimamia kuendeleza hamasa ya kutekeleza agenda hii muhimu.
"Nikuombe Katibu Mkuu uweke utaratibu mzuri wa Makundi tunayoyasimamia na hata Watumishi wa Wizara wanaposheherekea kumbukumbu za Siku zao za Kuzaliwa pia wapande miti ili kuendeleza agenda hii kwenye vizazi" amesema Dkt. Gwajima
Aidha amesisitiza zoezi hilo kuendelezwa katika Makazi ya Wazee, Makao ya Watoto na maeneo mbalimbali ambayo Wizara inayasimamia makundi hayo.
Naye Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amesema Wizara itasimamia agenda hiyo kwa kuhakikisha inayaratibu Makundi inayosimamia na Watumishi wake kuwahamasisha kuadhimisha siku zao za kuzaliwa pia kwa kupanda Miti kama ilivyoagizwa ili kuunga mkono maono ya Rais Samia ya kuwa endelevu katika kulinda na kutunza mazingira.
Zoezi la upandaji Miti mbele ya Ofisi ya Waziri Mtumba Jijini Dodoma limehusisha Menejimenti na Watumishi wa Wizara hiyo.