WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA KITUO CHA HUDUMA KWA MANUSURA WA UKATILI (ONE STOP CENTER) TARIME

Na WMJJWM - Tarime- Mara
Serikali imeendelea kuchukua hatua madhubuti katika mapambano dhidi ya ukatili wa kijinsia kwa kuimarisha mifumo ya huduma kwa manusura ikiwemo kuanzisha Vituo vya huduma Jumuishi katika maeneo mbalimbali nchini.
Akizindua mmoja ya Kituo hicho katika Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, mkoani Mara Februari 8, 2025 Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amesema kuwa Serikali imeimarisha sheria kupambana na ukatili wa kijinsia, hususan ukeketaji ikiwemo Sheria ya Mtoto, Sura ya 13, Kifungu cha 158A, inatoa adhabu kali kwa wahusika wa ukeketaji, ikiwa ni faini ya shilingi milioni 2 au kifungo cha miaka 5 hadi 15.
Pia amesema katika Sheria hiyo Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16, Kifungu cha 169A (2), inabainisha kuwa yeyote anayeshiriki ukeketaji anaweza kupewa adhabu ya kifungo cha miaka 5 hadi 15 au faini isiyozidi shilingi milioni 1, au vyote kwa pamoja, pamoja na kulipa fidia kwa manusura wa ukatili huo huku akisisitiza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha vitendo vya ukeketaji vinatokomezwa kabisa.
"Natoa wito kwa mikoa yenye viwango vikubwa vya ukeketaji, ikiwemo Mara, Arusha, Tanga, na Iringa, kuhakikisha inatenga bajeti maalum kwa afua za kupinga ukeketaji na kutoa huduma bora kwa manusura wa ukatili," amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Bunda Mhe. Dkt. Vincent Naano, ameishukuru UNFPA na Serikali ya Finland kwa ushirikiano wao na Serikali ya Tanzania katika kupambana na ukatili, hususan ukeketaji kwa kufanikisha ujenzi wa kituo hicho.
Aidha ameiagiza Halmashauri ya Wilaya ya Tarime kuhakikisha inajenga nyumba salama kwa watoto wanaokumbwa na ukatili kwa kutumia mapato ya ndani, ili kuimarisha ulinzi kwa waathirika wa vitendo vya ukatili wa kijinsia.
Naye Balozi wa Finland nchini Tanzania, Mhe. Theresa Zitting amesema kuwa ukatili wa kijinsia ni tatizo la dunia nzima na si Tanzania pekee, hivyo kuna umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali, jamii na wadau wa maendeleo katika mapambano hayo