WAZIRI DKT. GWAJIMA AZINDUA KITABU CHA UKATILI WA WANAWAKE KWA WANAWAKE - Hali Halisi ya sasa na muelekeo wa baadaye.

Dar Es Salaam
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima amezindua kitabu kiitwacho UKATILI WA WANAWAKE KWA WANAWAKE TANZANIA:HALI HALISI YA SASA NA MUELEKEO WA BAADAYE.
Akizindua kitabu hicho katika hafla iliyoandaliwa na Taasisi ya utafiti ya REPOA, Julai 18, 2024 jijini Dar Es Salaam, Waziri Dkt. Gwajima ametoa wito kwa wadau kuchukua hatua za kibunifu ili kuhakikisha ukatili wa kijinsia unamalizika nchini Tanzania.
Waziri Dkt. Gwajima amesema uzinduzi wa kitabu hicho utakuwa ni fursa nzuri ya kupendekeza sera zitakazofanya jamii yenye amani na kwamba Serikali itashirikiana kwa karibu na wadau kwa manufaa ya jamii yote.
Amebainisha kuwa, kushughulikia masuala ya ukatili wa kijinsia ndio msingi wa mipango yote ya maendeleo ya taifa ya muda mfupi, muda wa kati na muda mrefu kwa sababu unyanyasaji wa kijinsia ni ukiukaji mkubwa wa haki za binadamu na suala linalohatarisha maisha ya afya na ulinzi.
"Ninaipongeza REPOA kwa kuweka masuala ya jinsia na maendeleo ya kijamii miongoni mwa ajenda muhimu za utafiti kwa kuandaa warsha za midahalo ili kusambaza matokeo" amesema Waziri Dkt. Gwajima.
Waziri Dkt. Gwajima amesema katika kukabiliana na changamoto hiyo ya ukatili kwa wanawake, Serikali inafanya juhudi ili kuchochea ubunifu wenye uwiano ikiwemo kuimarisha mazingira ya kisheria ya kuwalinda wanawake walionyanyaswa, na uwekezaji wa miundombinu wezeshi ya kiuchumi kama shule, hospitali na barabara.
Aidha, amebainisha kwamba, mageuzi mbalimbali yanaendelea hasa katika sekta ya uchumi kupitia taasisi za elimu na mafunzo katika ngazi mbalimbali ambayo ni pamoja na kuwawezesha wanawake kujitegemea kwa kuwapatia ujuzi wa ujasiriamali, upatikanaji wa mikopo na uhamasishaji wa fedha za kuwaweka kwenye makazi salama wanawake walioathiriwa na ukatili.
Ameongeza kuwa, kwa kuzingatia mila potofu, majukumu ya kijinsia na athari za mfumo dume, hafla hiyo inalenga kuwapa uwezo wasomi, wanaharakati, watunga sera, viongozi wa no Serikali na wanajamii kushughulikia changamoto hizo kwa pamoja ambapo matokeo yatakayowasilishwa yatatoa mchango muhimu katika kubuni michakato ya kisera kuwezesha uelewa juu ya UKATILI WA WANAWAKE JUU YA WANAWAKE TANZANIA na kukuza Mahusiano ya Kijamii yenye uwiano.