WAZIRI DKT. GWAJIMA ATOA ZAWADI ZA HERI YA MWAKA MPYA KWA WAZEE NA WATOTO KWA NIABA YA MHE. RAIS DKT. SAMIA
Na WMJJWM – DAR ES SALAAM
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kutoa zawadi za Heri ya Mwaka Mpya 2026 kwa wazee na watoto kupitia Makao ya Watoto ya Huruma na Makao ya Wazee ya Tushikamane Pamoja Foundation (TPF), yaliyopo Manispaa ya Ubungo, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa kukabidhi zawadi hizo leo Januari 05, 2026, Waziri Dkt. Gwajima amesema kuwa ziara yake katika makao hayo ni kielelezo cha dhamira ya dhati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya kuhakikisha ustawi, ulinzi na maendeleo ya watoto, wazee na makundi yote maalum, ambayo yanaendelea kupewa kipaumbele cha juu. Amesema kuwa vituo hivyo vinawakilisha vituo vingine vyote nchini katika zoezi hilo la utoaji wa zawadi.
“Napenda kutumia fursa hii kuwaeleza kuwa zawadi hizi za sikukuu za mwisho wa mwaka ninazokabidhi leo, nazitoa kwa niaba ya Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan. Mheshimiwa Rais ana upendo mkubwa kwa watoto na wazee, na anaendelea kuhakikisha ustawi na maendeleo yenu. Zawadi hizi ni ishara ya upendo wake, matumaini na imani aliyonayo kwenu kama Taifa la leo na kesho,” amesema Dkt. Gwajima.
Kwa upande wake, Kamishna wa Ustawi wa Jamii, Dkt. Nandera Mhando, amesema kuwa Wizara, kwa kushirikiana na Maafisa Ustawi wa Jamii, itaendelea kutembelea na kufuatilia kwa karibu vituo vya makao ya watoto na wazee ili kusikiliza changamoto zao moja kwa moja na kuzitafutia ufumbuzi wa kudumu.
Nao watoto na wazee wa makao hayo wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pamoja na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, kwa upendo na zawadi walizopokea, na wamemtakia Mheshimiwa Rais Heri ya Mwaka Mpya 2026, wakimuombea afya njema, amani na mafanikio katika kuendelea kuliongoza Taifa.