WAZIRI DKT. GWAJIMA ATOA WITO WAHITIMU VYUO VYA MAENDELEO YA JAMII KUISAIDIA JAMII

Iringa
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito kwa wahitimu wa Taaluma ya Maendeleo ya Jamii kurudi kwenye jamii na kusaidia kubadili fikra kwa kutumia taaluma zao.
Ametoa wito huo wakati akizungumza na wanachuo na wananchi wanaozunguka chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha Julai 16, 2024 mkoani Iringa kwenye ziara yake ya kutembelea vyuo vya Maendeleo ya Jamii.
"Kama sisi tuna Maafisa Maendeleo ya Jamii 10461 waliosomeshwa na wana uwezo wa kubadilisha fikra za jamii na wako kwenye jamii, kuna programu gani zinazofanyika kukarabati jamii na kukabiliana na changamoto za ukatili" amehoji Waziri Gwajima.
Amesema wataalamu wa Ustawi na Maendeleo ya jamii wana haja ya kuona kwamba ni wajibu wao kuwa na miradi itakayobadili fikra na kuwajenga watoto kuwa na utu na maadili mema katika jamii.
Ameongeza kuwa, wataalamu hao wana uwezo wa kujadili changamoto za maadili zilizopo katika jamii kama ilivyo changamoto nyingine za afya, maji, elimu au barabara.
Kwa upande wake mkuu wa chuo cha Maendeleo ya Jamii Ruaha Godgrey Mafungu akitoa taarifa ya chuo hicho, amebainisha kuwa tangu kimeanzishwa kimedahili wanafunzi 10,461 ambapo amesema chuo kimekuwa na mchango mkubwa kwa Taifa kwa kuzalisha wataalamu wa maendeleo ya jamii.