WAZIRI DKT. GWAJIMA AHIMIZA UWAJIBIKAJI KWENYE KUIMARISHA MAJUKWAA YA UWEZESHAJI WANAWAKE KIUCHUMI.
Na WMJJWMJ – Morogoro
Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe.Dkt. Dorothy Gwajima, amewataka waratibu na viongozi wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kuongeza uwajibikaji ili majukwaa hayo yawe na matokeo makubwa zaidi.
Dkt. Gwajima ametoa kauli hiyo katika kikao cha majukwaa hayo kilichofanyika Machi 3, 2026 mkoani Morogoro, ambapo alijionea maendeleo ya utekelezaji wa majukwaa hayo na kupokea taarifa za uwezeshaji wanawake kiuchumi mkoani humo.
Ameipongeza Kata ya Kilakala kwa kuunda jukwaa la kata lenye jumla ya vikundi 40 vya wanawake huku akisisitiza umuhimu wa kuongeza hamasa ili wanawake wengi zaidi wajumuishwe.
Vilevile, Dkt. Gwajima amesisitiza umuhimu wa ajenda ya majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kumilikiwa kikamilifu kama ajenda ya maendeleo kwenye vikao rasmi vya halmashauri ngazi zote.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Morogoro, Mhe. Mussa Kilakala, amesema Mkoa wa Morogoro utaendelea kutekeleza ajenda ya uwezeshaji wanawake kiuchumi kwa kutoa elimu kwa wanawake ili kujiunga na majukwaa hayo bila ubaguzi wa aina yoyote.
Aidha, Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Maendeleo ya Jinsia, Juliana Kibonde, amesema Serikali kupitia Wizara ya Maendeleo ya Jamii itaendelea kuratibu na kusimamia majukwaa hayo, kutoa elimu pamoja na kuhakikisha hakuna mwanamke anayebaki nyuma katika kunufaika na fursa za kiuchumi.