Habari

Imewekwa: Dec, 10 2021

WATAALAM WA MAENDELEO YA JAMII WAASWA KUENDELEA KUSAIDIA JAMII

News Images

Wataalam wa Maendeleo ya Jamii nchini wametakiwa kuendelea kutumikia wananchi katika kuhakikisha utaalam wao unaendelea kusaidia jamii na nchi katika utekelezaji wa Sera mbalimbali.

Hayo yamebainika katika mjadala wa Wazi uliofanyika katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru uliongozwa na mada isemayo Mchango wa Taaluma ya Maendeleo ya Jamii kwa miaka 60 ya Uhuru.

Akizungumza katika Mjadala huo Mkuu wa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru, Dkt. Bakari George amesema lengo la mjadala huo ni kubadilisha mawazo na kupata mawazo ya namna ya Watalaam wa Maendeleo ya Jamii wanavyoweza kutumika katika jamii.

Dkt. Bakari George amesema kuwa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wamekuwa wakitumika tangu enzi za kupata uhuru katika kutekeleza Sera na Mipango mbalimbali hasa kubadili fikra za wananchi katika kujiletea maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.

"Taaluma ya Maendeleo ya Jamii wakati huo baada ya Uhuru kwani Baba wa Taifa Julius Nyerere aliwatumia wataalam hawa katika kuelimisha Jamii katika Sera ya ujamaa na kujitegemea" alisema Dkt Bakari

Ameongeza kuwa Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru inaendelea kuhakikisha inazalisha Watalaam wa Maendeleo ya Jamii wenye uwezo na ari kubwa ya kuisaidia Jamii katika kupambana na changamoto mbalimbali zinazoikabili.

Naye rais wa Chama Cha Maendeleo ya Jamii (CODEPATA) Bi Anjela Mvaa amesema Watalaam wa Maendeleo ya Jamii ni watu muhimu katika kuielimisha jamii katika kuondoka na matatizo mbalimbali hasa kujikwamua kichumi kwa kuwasaidia kupata fursa za Maendeleo.

"Katika utendaji kazi wetu Wataalam wa Maendeleo ya Jamii tunatumika katika utekelezaji wa Sera na Mipango ya nchi hivyo ni kada ambayo inahitaji kuangalia katika kuwezeshwa kuifikia Jamii " alisema Bi Anjela

Ameongeza kuwa sekta ya Maendeleo ya Jamii imesaidia Jamii kujitambua katika kusimamia na kuchangia katika utekelezaji wa miradi au mabadiliko ya Sera na Mipango mbalimbali ya nchi.

Kwa upande wake Mwakilishi kutoka Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) Patient Abraham amewashauri Watalaam wa Maendeleo ya Jamii kuendana na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano katika kuhakikisha wanaongea ubunifu katika utekelezaji wa majukumu yao katika jamii.

" Ubunifu ni muhimu sana katika masuala mbalimbali na katika hili la Maendeleo ya Jamii suala la ubunifu ni muhimu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuendana na mabadiliko ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano" alisema Bi. Patient

Akichangia mada katika Mjadala huo wa Wazi Lusajo Kamwela amesema kuwa Wataalam wa Maendeleo ya Jamii wanamchango mkubwa katika kusaidia jamii kwa kushirikiana na Idara nyingine za Serikali katika kutoa huduma kwa wananchi katika maeneo yao.