Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WANAWAKE WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UCHUMI NA KULINDA HAKI ZA WATOTO WENYE ULEMAVU.

Imewekwa: 06 Mar, 2026
WANAWAKE WATAKIWA KUCHANGAMKIA FURSA ZA UCHUMI NA KULINDA HAKI ZA WATOTO WENYE ULEMAVU.

Na Jackline Minja, WMJJWM

Mbeya

Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Mhandisi Maryprisca Mahundi amesema Serikali itaendelea kusimamia haki za wanawake na wasichana pamoja na kuwawezesha kiuchumi ili kuhakikisha wanashiriki kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.

Mhandisi Mahundi amesema hayo Leo tarehe 06 Machi 2026, katika kongamano la wanawake lililofanyika Ukumbi wa Mkapa, Jijini Mbeya ikiwa ni kuelekea kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Wanawake Machi 8, 2026. Kauli mbiu ya mwaka huu inahimiza haki kwa wanawake na wasichana kama msingi wa maendeleo jumuishi kufikia Dira ya Taifa ya 2050.

“Serikali itaendelea kusimamia na kulinda haki za wanawake na wasichana ili kuhakikisha wanapata fursa sawa katika elimu, uchumi na uongozi. Ni wajibu wa jamii nzima kuhakikisha mwanamke wanathaminiwa na kupewa nafasi ya kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla.”

Aidha, Mbunge wa Viti Maalum Mhe. Nassirya Nassir Ally amewataka wazazi na walezi kuwatunza watoto wote bila ubaguzi, hususan watoto wenye ulemavu, huku akisisitiza kuwa kuwaficha watoto hao kunawanyima haki zao za msingi na fursa za kuonesha vipaji na uwezo walionao katika jamii.

“Nitoe wito kwa wazazi na walezi kuacha tabia ya kuwaficha watoto wenye ulemavu, Watoto hawa wana uwezo mkubwa kama watoto wengine na wakipewa malezi bora, elimu na mazingira rafiki wanaweza kufanya mambo makubwa na kuisaidia jamii na Taifa letu.”

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Justice Laurent Kijazi amewahimiza wanawake kuchangamkia fursa za mikopo inayotolewa na Serikali kupitia asilimia 10 ya mapato ya halmashauri kwa vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kukuza mitaji yao na kuboresha maisha ya familia zao.

Kongamano hilo limewakutanisha wanawake kutoka makundi mbalimbali, viongozi wa Serikali, wadau wa maendeleo pamoja na wananchi kwa lengo la kujadili masuala ya haki za wanawake, usawa wa kijinsia, ujasiriamali na kupinga vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii.