WANAWAKE WANUFAIKA WA WDF DODOMA WAONESHA MATOKEO CHANYA YA MIKOPO YA SERIKALI
WANAWAKE WANUFAIKA WA WDF DODOMA WAONESHA MATOKEO CHANYA YA MIKOPO YA SERIKALI
Na Jackline Minja WMJJWM-
Dodoma
Wanawake walionufaikana Mkopo unaotolewa na Mfumo wa Maendeleo ya Wanawake wameonesha matokeo chanya katika shughuli wanazifanya kutokana na Mkopo waliupaya kupitia Mfuko huo.
Hayo yamebainika wakati huu a ziara ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, leo Desemba 16, 2025 alipotembelea miradi ya wanawake wanufaika wa Mikopo ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake (WDF) jijini Dodoma.
Akizungumza mara baada ya kukamilisha ziara hiyo, Mdemu amesema ameridhishwa na hatua iliyofikiwa na miradi hiyo akieleza kuwa inaonesha wazi dhamira ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kuwawezesha wanawake kiuchumi kupitia Mikopo ya Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake.
Amesema miradi aliyotembelea, ikiwemo kiwanda cha Carls’ Plastic cha uchakataji wa chupa za plastiki, kiwanda cha uchujaji wa mafuta ya alizeti pamoja na duka la dawa muhimu, imeonesha matumizi sahihi ya mikopo hiyo na uwezo wa wanawake katika kuendesha miradi yenye tija na inayochangia ajira na kipato.
“Miradi hii inaonesha kuwa mikopo ya WDF inaleta matokeo chanya pale inapotumika kwa malengo yaliyokusudiwa. Hii ni fursa kwa wanawake na vijana wengine kujifunza na kujitokeza kuchangamkia mikopo hii na tukumbuke fedha hizi ni za mzunguko, hivyo urejeshaji kwa wakati unatoa nafasi kwa wanawake wengine wengi zaidi kunufaika na mfuko huu,” amesema Mdemu.
Kwa upande wao, wanufaika wa mikopo hiyo wameipongeza Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wanawake na vijana kupitia mikopo yenye masharti nafuu ambapo imewawezesha kuanzisha na kupanua biashara zao, kuongeza ajira na kuboresha maisha ya familia zao.
“Mikopo ya WDF imetuwezesha kufanya kazi na kuongeza kipato. Tunawahimiza wanawake na vijana wengine kuchangamkia fursa hizi na kutumia mikopo kufanya kazi badala ya kubweteka,” amesema mmoja wa wanufaika.
Wanufaika hao wameahidi kuendelea kusimamia miradi yao kwa ufanisi na kurejesha mikopo kwa wakati ili wanawake wengi zaidi wanufaike na Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake kwa maendeleo yao na Taifa kwa ujumla.
MWISHO