Habari

Imewekwa: Mar, 27 2023

​WANAWAKE WAHIMIZWA KUJIUNGA NA MAJUKWAA

News Images

Wito umetolewa kwa Wanawake kujiunga na majukwaa ya uwezeshaji kiuchumi Ili kujadili na kufahamishana kuhusu fursa za Maendeleo na uchumi.

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima ametoa wito huo akihitimisha ziara yake ya siku mbili mkoani Tabora iliyolenga kufuatilia utekelezaji wa Sera na Mipango inayosimamiwa na Wizara hiyo Machi 25-26, 2023.

Waziri Dkt. Gwajima amesema Majukwaa hayo yanawawezesha Wanawake kujiimarisha kiuchumi na kujitegemea hivyo kuwaepusha na changamoto ya ukatili wa kijinsia kwa kutokuwa tegemezi.

Ametoa maelekezo kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii kutoa mafunzo kwa viongozi wa majukwaa hayo ili kuwajengea uwezo yafanye kazi kikamilifu.

"Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake kiuchumi ni sehemu inayowaweka Wanawake pamoja ili wajadili na kupeana taarifa ya fursa za kiuchumi zilizopo na changamoto zinazowakabili Ili kuja na ufumbuzi, majukwaa haya aliyaasisi Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tangu akiwa Makamu wa Rais na ajenda hii inaendelea. Wanawake wakiwa kwenye majukwaa ni rahisi kuwafikia" amesema Dkt. Gwajima.

Aidha, Waziri Dkt. Gwajima ametumia nafasi hiyo kuwakumbusha viongozi wa mamlaka za Serikali za Mitaa kushirikiana na wananchi kutatua changamoto ndani ya Jamii kupitia mifumo iliyowekwa ili kuwalinda watoto dhidi ya ukatili.

Amesema Kamati za ulinzi wa Wanawake na Watoto ngazi ya vijiji na Mitaa zina uwezo wa kuibua na kutatua changamoto ya vitendo vya ukatili iwapo zitafanya kazi yake kikamilifu ambapo taarifa ya wilaya ya Sikonge iliyowasilishwa na Kaimu Katibu Tawala wa wilaya hiyo Rosina Swai inasema kwa kipindi cha 2022-2023 watoto wa kike 34 wameacha shule kutokana na mimba za utotoni na kwamba watoto 1059 hawapo shuleni kwa utoro.

Vilevile, Waziri Dkt. Gwajima amewaelekeza Maafisa Maendeleo ya Jamii kuhakikisha takwimu za kundi la Wajane na Yatima zinapatikana kabla ya mwezi Juni kwa lengo la kutambua idadi yao na kuwezesha Uratibu wao.

Kuhusu wafanyabiashara ndogo ndogo maarufu kama machinga, Waziri Dkt.Gwajima amezishauri Mamlaka za Serikali za Mitaa kukaa na kuzungumza na kundi hilo Ili ubaini changamoto zao hususani maeneo ya kufanyia biashara.

Ameupongeza mkoa wa Tabora kwa juhudi zake kuhakikisha kila Wilaya machinga wametengewa maeneo katikati ya miji hivyo kurahisisha mazingira mazuri ya biashara.

Akizungumzia Mashirika Yasiyo ya Kiserikali amesema Wadau ni muhimu kushirikishwa katika maeneo yote ili kutoa mchango wao katika kuendeleza Jamii.

Katika ziara yake Waziri Gwajima amekutana na Makundi ya Wajane, machinga, mabaraza ya wazee, mabaraza ya watoto, majukwaa ya uwezeshaji Wanawake kiuchumi na Kamati

za MTAKUWWA katika Halmashauri ya Wilaya Sikonge na Halmashauri ya Manispaa ya Tabora.

Kwa upande wao baadhi ya wananchi katika mkutano hiyo wameipongeza Serikali hasa Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa jitihada zake za kuhakikisha anaimarisha Ustawi na Maendeleo ya Jamii na kuunda wizara Maalum.

"Rais Samia ni kiongozi wa mfano tunazidi kumpongeza hasa sisi Wanawake wa mkoa wa Tabora, tangu aanzishe Wizara hii tumetambuliwa na wewe Mhe Waziri umekuwa bega kwa bega na sisi' amesema Ashura Mazembe Katibu wa Jukwaa la Wanawake mkoa wa Tabora.

MWISHO