WANAWAKE KUWEZESHWA KATIKA MATUMIZI YA TEHEMA - NAIBU KATIBU MKUU MPANJU.

Na WMJJWM - Dodoma
Serikali ya Tanzania inaendelea kushirikiana na Serikali ya Ujerumani katika uhamasishaji wa wanawake kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano ili kukuza ujuzi pamoja na kujijenga wenyewe na kuleta usawa wa kijinsia.
Hayo yamesemwa Aprili 16, 2025 jijini Dodoma na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Wakili Amon Mpanju, wakati wa kikao kazi na wawakilishi kutoka Ubalozi wa Ujerumani kujadili mashrikiano katika mradi wa kuhamasisha wanawake kutumia teknolojia ya habari na mawasiliano (TEHAMA), kwa maendeleo yao.
Wakili Mpanju amesema lengo la Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Mhe. Dkt. Samia Hassan Suluhu ni kuhakikisha Wanawake wanapata fursa sawa za kidigitali, usawa wa kijinsia ikiwa ni pamoja na kushiriki ipasavyo katika matumizi ya teknolojia ya Tehama.
Amesema kwamba ,Wizara ipo katika maandalizi ya kuingia makubaliano na Serikali ya Ujerumani juu ya kuwezesha wanawake na wasichana katika ubunifu wa kiteknolojia, matumizi ya akili mnemba ili kuwa na uwezo wa kutatua changamoto mbalimbali za kijamii.
Kwa upande wake Mwakilishi kutoka ubalozi wa Ujerumani
Julia Kronberg amesema mradi huo utahusu kuimarisha utaalam wa Kidijitali kwa wanawawke kutumia mbinu za kidijitali katika nyanja za usawa wa kijinsia na haki za binadamu.
Ameongeza kwamba mradi huo utahusisha Mashirika ya kijamii, vyuo vikuu, na kampuni zinazoinukia ambazo zinazoendeshwa na wanawake, ambapo watapewa mafunzo ya uzalishaji wa bidhaa mbalimbali Kama vile zile zinazotokana na ngozi, huduma za uchapishaji bidhaa kwa kutumia mashine ambazo zinatumia mali ghafi zinazolinda mazingira.