Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

WANAUME WANA NAFASI KUBWA YA KUTOMEZA UKATILI WA KIJINSIA - DKT. TULIA

Imewekwa: 11 Mar, 2025
WANAUME WANA NAFASI KUBWA YA KUTOMEZA UKATILI WA KIJINSIA - DKT. TULIA

Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani Dkt. Tulia Ackson amewataka wanaume kuwa mstari wa mbele kuleta mabadiliko ya usawa wa kijinsia kwa kushiriki kwenye masuala mtambuka ikiwemo mapambano dhidi ya udumavu, ukatili wa kijinsia na malezi ya watoto.

Dkt. Tulia amebaini hayo katika  kongamano la wanawake la  kanda za nyanda ya juu kusini Machi 05, 2025, jijini Mbeya.

Amesema tafiti zimebaini kuwa mataifa ambayo yamewahusisha wanaume kikamilifu katika kampeni mbalimbali, ikiwemo zile za lishe bora, yamefanikiwa kwa kiwango kikubwa kukabiliana na changamoto zinazoikumba jamii lakini katika Jamii zetu tafiti zinaonesha ushiriki wa wanaume bado ni mdogo hivyo kusababisha mabadiliko ya usawa wa kijinsia na maendeleo kwa ujumla kuwa kidogo.

“Hatuwezi kutegemea juhudi za wanawake na Serikali pekee wanaume pia mnayo nafasi kubwa katika kubadilisha mwelekeo wa jamii yetu na ni lazima  tufahamu kuwa ukatili wa kijinsia hautatokomea, na uwezeshaji wa wanawake kiuchumi hautafanikiwa, ikiwa hatutachukua hatua madhubuti kama jamii kwa ujumla hivyo nategemea kuona idadi kubwa ya wanaume wakitoa ushirikiano wa hali ya juu” amesema Dkt Tulia.

Vilevile Dkt Tulia ametoa wito kwa wanawake kujiunga na Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi kwa lengo la kuwawezesha wanawake kupata mafunzo ya biashara, kukuza mitandao ya kibiashara, na kushiriki katika shughuli za kiuchumi.

“ Hadi kufikia Desemba 2024, majukwaa haya yalikuwa tayari yamesambaa katika Mikoa 26, Halmashauri 152 kati ya 184, Kata 1,354 kati ya 3,957 na Mitaa/Vijiji 1,859 kati ya Vijiji 12,318" Amesema DKT. Tulia.

Aidha Dkt Tulia ametoa rai  kwa watanzania wote, wanawake kwa wanaume kurasimisha biashara zao ili kunufaika na fursa mbalimbali ikiwemo ya kufanya biashara Barani Afrika ambapo masharti yasiyo ya kiushuru yamepunguzwa kupitia Utekelezaji wa Mkataba wa AfCFTA unafungua milango ya soko la pamoja la zaidi ya watu Bilioni 1.3 barani Afrika.