Habari

Imewekwa: Jul, 27 2022

VIONGOZI TUWE TAYARI KUIBUA VIPAJI VYA WATOTO: WAZIRI DKT. GWAJIMA

News Images

VIONGOZI TUWE TAYARI KUIBUA VIPAJI VYA WATOTO: WAZIRI DKT. GWAJIMA

Viongozi wanawake wametakiwa kuwa mstari mbele kuibua na kuendeleza vipaji vya watoto ambavyo vimekuwa vikipotea kutokana na madhila wanayoyapitia au kutotambuliwa na jamii inayowazunguka.

Waziri Dkt. Gwajima ameyasema hayo Julai 26, 2022 wakati wa warsha ya kuboresha haki za wanawake na vijana iliyoandaliwa na Chama cha Wanawake Wanasheria (TAWLA) mkoani Dar es Salaam, ambapo amesema wamebaini hata vijana ambao wamekimbia kwa wazazi wao wapo wenye vipaji lakini wanakosa watu wa kuwashika mkono ili waweze kufikia ndoto zao.

“Nitumie fursa hii kuwaomba viongozi wenzangu, tuwe daraja la kubaini vipaji ili kesho na kesho kutwa tuje kuwa na vipaji vingi zaidi nchini vitavyogeuka ajira na kuwapatia kipato.

"Kuna watu Mungu amewaumba wao kazi yao ni Sanaa ya kuburudisha, hivyo pamoja na kuwarejesha shuleni wapate elimu, tuwaibue ili vipaji vyao viimarike waweze kuja kutengeneza ajira kwa watu wengine” alisema Dkt. Gwajima

Dkt. Gwajima amesema wapo watoto wengi wanaishi kwenye mazingira magumu ambapo huko hufanyiwa ukatili, hivyo akakitaka Chama hicho kujiunga na Kampeni huru ya Shujaa wa Maendeleo na Ustawi wa Jamii, SMAUJATA ambayo toka kuzinduliwa kwake imesha fikisha mashujaa 7000 katika ngazi mbali mbali ikiwepo Vijijini.

“Rais wetu Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa ya kuunda Wizara, lakini pamoja na hivyo ameweka fursa nyingi katika maeneo mengi ya nchi hivyo, swali la kujiuliza kwa nini basi wapo wanaokimbilia mijini na wakifika mijini wanaishi kwenye mazingira hatarishi, lazima tuungane na SMAUJATA, ili vita hivi vya kupinga ukatili tuweze kuvishinda" alisisitiza Waziri Gwajima

Dkt. Gwajima ameongeza pia kuwa, kundi la wanawake na mabinti ni muhimu sana katika maendeleo ya Taifa lolote na hapa nchini, takwimu zinaonesha, wanawake ni 51.04% na ambao hufanya kazi za nyumbani, kazi za uzalishaji shambani kiasi kwa 80% ya nguvu kazi ya Sekta ya kilimo aidha ni wanawake ambao huzalisha 60% ya chakula chote hapa nchini akawataka wanapoangalia mabadiliko hayo na uchechemuzi wa kumuinua mwanamke lazima wazingatie maeneo yote hayo.

Awali akimkaribisha Waziri Dkt. Gwajima, Mkurugenzi Mtendaji wa TAWLA, Tike Mwambipile, amemshukuru Waziri na kumpongeza kwa kazi anazozifanya, huku akihimiza Wanawake kujengewa nguvu za kiuchumi, lakini wajitahidi kuingia kwenye nafasi za maamuzi ili kupigania haki zao sambamba na Mifumo ya utoaji haki kuangaliwa upya kwenye utoaji wa haki za wanawake.