Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

VIONGOZI NA WADAU MKOA WA MARA WAJA NA MKAKATI MADHUBUTI WA KUKOMESHA UKEKETAJI

Imewekwa: 10 Feb, 2025
VIONGOZI NA WADAU MKOA WA MARA WAJA NA MKAKATI MADHUBUTI WA KUKOMESHA UKEKETAJI

VIONGOZI NA WADAU MKOA WA MARA WAJA NA MKAKATI MADHUBUTI WA KUKOMESHA UKEKETAJI

Na WMJJWM - Mara

Mkuu wa Polisi Jamii wa Tarime-Rorya, ACP Jumanne Mkwama amesema jumla ya kesi 1,131 za ukatili wa kijinsia zimeripotiwa katika Dawati la Jinsia na Watoto wilayani humo kwa mwaka 2024, ambapo kufuatia taarifa hizo Jeshi la Polisi limeongeza juhudi za kudhibiti matukio hayo mkoani Mara.

ACP Mkwamba amesema hayokatika madhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukeketaji dhidi ya Wanawake na Watoto wa Kike ambayo kitaifa yamefanyika Februari 6, 2025, wilayani Tarime mkoani Mara.

ACP Mkwamba amesisitiza jamii kutokufumbia macho matukio ya ukatili, na kwamba jeshi la polisi limejipanga kutoa elimu zaidi kwa wazazi, wazee wa kimila, na jamii kwa ujumla kuhusu madhara ya ukeketaji ili kuongeza mwamko wa kuripoti vitendo hivyo na hatimaye kuvimaliza kabisa.

Katika maadhimisho hayo wadau walijadili mikakati madhubuti ya kutokomeza ukatili wa kijinsia, hususan ukeketaji, ambapo wamependekeza hatua kadhaa kuchukuliwa ili  kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ukatili huo.

Miongoni mwa mapendekezo ni kuanzishwa kwa programu maalum za kutoa elimu  shuleni kuhusu madhara ya ukeketaji ili kukuza uelewa na kuondoa mila hiyo potofu. Vilevile, walipendekeza kuwepo kwa adhabu kali kwa yeyote atakayebainika kushiriki katika vitendo vya ukeketaji.

Kwa upande wake, Mratibu wa Kampeni ya Kutokomeza Ukeketaji nchini, Denis Moses, ameeleza kuwa ushirikiano wa jamii nzima ikiwemo watoto, wazazi, Mashirika yasiyo ya Kiserikali, Wazee wa mila, na viongozi wa dini ni msingi imara wa kufanikisha mapambano dhidi ya ukeketaji.

Naye Afisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Mara, Elizabeth Mhenya amesema kuwa Mkoa wa Mara umejipanga kuendelea kupunguza na hatimaye kutokomeza ukeketaji kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kutoa elimu kwa jamii, kuendesha kampeni za uhamasishaji, na kuongeza juhudi za kupinga ukatili wa kijinsia.