TUWALINDE WATOTO DHIDI YA ATHARI ZA MATUMIZI YA MITANDAO: Dkt Jingu
TUWALINDE WATOTO DHIDI YA ATHARI ZA MATUMIZI YA MITANDAO: Dkt Jingu
Na Abdala Sifi WMJJWM- Dodoma
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. John Jingu amesema wazazi, walezi na jamii kwa ujumla wanalo jukumu la kuhakikisha Watoto wanalindwa dhidi ya madhara yatokanayo na matumizi yasiyo sahihi ya mitandao.
Dkt Jingu amesema hayo wakati akifungua kikao cha cha Kamati ya Kitaifa ya ushauri kuhusu usalama wa Mtoto mtandaoni, kilichofanyika Jijini Dodoma tarehe 26 Novemba, 2025.
“Mzazi anapaswa kuhakikisha mtoto wake anakuwa salama katika matumizi ya mitandao, ili kuepuka hatari zinazoweza kuwapata kama vile kurubuniwa, kunyanyaswa na vitendo vingine vya kikatili” amesema Dkt Jingu.
Dkt Jingu amepongeza Kamati hiyo kwa utekelezaji wa mipango na mikakati na kampeni mbalimbali kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa kuhusu usalama wa mtoto mtandaoni na kuitaka kuongeza nguvu katika kutoa elimu kupitia majukwaa na kwa njia tofauti ili kuifikia jamii nzima.
Awali akizungumza katika kikao hicho Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya mtoto kutoka Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Sebastian Kitiku amesema kila mtu kwa nafasi yake anapaswa kuchukua hatua kukabiliana na athari zinazotokana na matumizi yasiyo sahihi kwa Watoto.
Ameongeza kwamba wazazi wengi hupenda kuwabembeleza watoto wao kwa kuwapa simu pasina kuweka uangalizi, kitenda ambacho kinawapa nafasi ya kufikia maudhui yenye athari kwao.
Lengo la kikao cha robo cha Kamati ya Kitaifa ya ushauri kuhusu usalama wa mtoto mtandaoni ni kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji kutoka Serikalini na kwa wadau mbalimbali ambao wanashiriki katika kampeni mbalimbali za ulinzi na usalama wa mtoto mtandaoni.
MWISHO