Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

TATUENI CHANGAMOTO ZINAZOKABILI JAMII  KUPITIA FANI ZENU: DKT. NANDERA

Imewekwa: 19 Dec, 2025
TATUENI CHANGAMOTO ZINAZOKABILI JAMII  KUPITIA FANI ZENU: DKT. NANDERA

TATUENI CHANGAMOTO ZINAZOKABILI JAMII 
KUPITIA FANI ZENU: DKT. NANDERA 


Na Witness Masalu- WMJJWM Dodoma

Kamishna wa Ustawi wa Jamii Dkt. Nandera E Mhando ametoa wito kwa wahitimu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi-Decca kuchangamkia fursa zilizozopo katika jamii zao na kuwa sehemu ya utatuzi wa  changamoto kwa kutumia ujuzi na maarifa waliyopata kupitia taaluma zao.

Dkt Nandera ameyabainisha hayo katika Mahafali ya 9 ya chuo hicho alipomwakilisha Waziri wa  Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Mhe. Dkt Dorothy Gwajima Desemba 18, 2025 Mkoani Dodoma.

Dkt Nandera amesema Serikali inaendelea kufanya juhudi mbalimbali hususani kuimarisha sekta ya afya, kilimo na mifugo kwa lengo la kuleleta mazingira wezeshi kwa wananchi ikiwa ni pamoja na kupata huduma bora za afya karibu na maeneo yao.

“Jitihada hizo zinahusisha kuimarisha huduma za kinga ya magonjwa ikiwemo huduma za chanjo, huduma za lishe, huduma za usafi na afya ya mazingira, huduma za afya ngazi ya jamii, ujenzi wa hospitali na vituo vya kutolea huduma za afya, ongezeko la rasilimali watu katika sekta ya afya pamoja na mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza.”amesema Dkt Nandera.

Vilevile Dkt Nandera awewaasa Wahitimu wote kufanya kazi kwa bidii na kwa ufanisi mkubwa ili waweze kuendana na kasi ya mabadiliko ya dunia ya sasa kwani safari baada ya kuhitimu ina changamoto mbalimbali hivyo  wajitayarishe kukabiliana nazo.

“Tumieni  taaluma na fani zenu kama fursa ya kujiajiri na kuwa wajasiliamali kwa lengo la kuongeza wigo wa ajira katika jamii na bahati nzuri Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum chini ya Dkt Dorothy Gwajima inasimamia wajasiriamali na kutoa mikopo kwa wanawake na wajasiriamali wadogowadogo “amesema Dkt Nandera.

Vilevile Dkt Nandera ameeleza kwamba Serikali imeendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Sekta ya umma na binafsi katika utoaji huduma za afya pamoja na kuanzisha mpango wa utekelezaji wa Sheria ya Bima ya Afya kwa wote.

Awali akizungumza Mwenyekiti wa Bodi ya Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi -Decca Dkt. Ezekiel Mpuya ameishukuru Serikali kwa kuonesha ushirikiano wa hali ya juu katika kuwasimamia na kuhakikisha Chuo hicho kinakua na kupiga hatua ili kuweza kutoa huduma kwa jamii na kuahidi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Serikali kwa kufuata miongozo na kanuni zilizowekwa.

Naye Mmoja wa wahitimu wa kozi ya famasia kutoka Chuo hicho Neema Lunguya ametoa hamasa kwa watoa huduma za kifamasia kutimiza wajibu wao na kuzingatia sheria na kanuni zilizowekwa kwa maslahi ya jamii kwa ujumla.

MWISHO