Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

TANZANIA YATOA WITO KWA JUMUIYA ZA KIMATAIFA KUTAMBUA MCHANGO WA WANAWAKE KATIKA VIWANDA.

Imewekwa: 28 Nov, 2025
TANZANIA YATOA WITO KWA JUMUIYA ZA KIMATAIFA KUTAMBUA MCHANGO WA WANAWAKE KATIKA VIWANDA.

TANZANIA YATOA WITO KWA JUMUIYA ZA KIMATAIFA KUTAMBUA MCHANGO WA WANAWAKE KATIKA VIWANDA.

 

Na WMJJWM- Riyadh, Saudi Arabia.

Tanzania imetoa wito kwa jumuiya kimataifa na Mashirika ya Kimataifa kushirikiana katika kuweka mifumo inayotambua mchango wa wanawake katika Maendeleo ya Viwanda.

Wito huo umetolewa na Balozi na Mwakilishi wa Kudumu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa, Vienna, Mhe. Naimi S.H. Aziz, alipomwakilisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano wa Ngazi ya Juu Kuhamasisha Utambuzi wa Mchango wa Wanawake katika Maendeleo ya Viwanda (High level Dialogue on Mobilizing Recognition of Women in Industries: Next Step) uliofanyika tarehe 25 Novemba, 2025 wakati wa Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO’s General Conference) unaoendelea jijini Riyadh, Saudi Arabia.

Akichangia mjadala huo kama mwanajopo (panelist), Balozi Naimi Aziz alieleza kuwa wanawake wana mchango mkubwa katika maendeleo ya viwanda, japo hawatambuliwi na kuwezeshwa ipasavyo.

Ameeleza kuwa, wanawake wanakabiliwa na changamoto mbalimbali katika kushiriki uchumi jumuishi wa viwanda ikiwa ni pamoaja na mifumo dume, ukosefu wa mitaji, teknolojia za uzalishaji na masoko. 

Amezisihi Serikali za Nchi Wanachama wa UNIDO na Mashirika ya Kimataifa kushirikiana katika kuimarisha upatikanaji wa fedha, ubunifu wa teknolojia na masoko kwa wajasiriamali wanawake; kuwajengea uwezo wa kiufundi na ujasiriamali; kuweka mifumo ya usawa wa kijinsia katika mipango ya maendeleo ya taifa; na kuimarisha uongozi shirikishi na mifumo ya maamuzi katika viwanda. 

Balozi Naimi Aziz anamwakilisha Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye Mkutano Mkuu wa 21 wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo ya Viwanda (UNIDO’s General Conference) uliaonza tarehe 23-27 Novemba, 2025 jijini Riyadh, Saudi Arabia.

Mkutano huo uliwaleta pamoja viongozi wa mataifa mbalimbali wanachama wa UNIDO na washirika wa maendeleo wa kimataifa unajadili mwelekeo mpya wa mapinduzi ya viwanda duniani, kuhamisisha uwekezaji, kuchochea maendeleo ya sekta binafsi, mchango wa wanawake katika maendeleo ya viwanda, na kuhamasisisha mchango wa viwanda vya uzalishaji katika maendeleo ya kiuchumi.

Mkutano huo pia ulihushuliwa na Naibu katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Felister Mdemu.