Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

TANZANIA YAIMARISHA USHIRIKIANO NA UMOJA WA ULAYA (EU) KATIKA KUPAMBANA NA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO

Imewekwa: 27 Feb, 2025
TANZANIA YAIMARISHA USHIRIKIANO NA UMOJA WA ULAYA (EU) KATIKA KUPAMBANA NA UKATILI DHIDI YA WANAWAKE NA WATOTO

Na WMJJWM
Dar es Salaam, 24 Februari 2025

Tanzania imeendelea kuthibitisha dhamira yake ya kuhakikisha usawa wa kijinsia na haki za wanawake kupitia ushirikiano thabiti na Jumuiya ya Ulaya (EU). Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Mhe. Dkt. Dorothy Gwajima, ameeleza hayo Leo tarehe 24 February 2925, baada ya kukutana na Kamati ya Maendeleo ya Bunge la Ulaya (DEVE) jijini Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, Waziri Gwajima ameeleza wajumbe wa kamati hiyo kuwa tangu uhuru, Tanzania imekuwa ikitekeleza sera na sheria zinazosimamia haki sawa kwa jinsia zote na kwa uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, nchi imekuwa kinara katika kuhimiza haki za wanawake kiuchumi na kupunguza ukatili wa kijinsia.

"Serikali yetu imetengeneza mifumo inayojumuisha Sera Mpya ya Taifa ya Jinsia na Maendeleo ya Wanawake, Mpango wa Kutokomeza Ukatili Dhidi ya Wanawake na Watoto, na Mfumo wa Wanawake, Amani na Usalama," amesema Dkt. Gwajima.

Amefafanua kwamba ushirikiano kati ya Tanzania na EU umekuwa na mchango mkubwa kupitia Mpango wa Mageuzi ya Kijinsia (Gender Transformative Action Programme), maarufu kama "Breaking the Glass Ceiling", ambao umesaidia kuimarisha usawa wa kijinsia na kuwawezesha wanawake kiuchumi.

Kwa mafanikio hayo Tanzania imekuwa mshiriki hai katika Mpango wa Usawa wa Kizazi (Generation Equality Forum), huku Rais Samia akiwa kinara wa muungano wa haki za kiuchumi kwa wanawake.

"Wakati tunasherehekea mafanikio haya, bado tunakabiliwa na changamoto. Tunashukuru kwa kuongezwa kwa muda wa miaka miwili kwenye programu inayolenga masuala ya jinsia na elimu, jambo linaloendana na Sera mpya ya Elimu iliyoanzishwa na Rais Samia," aliongeza.

Tanzania inatarajia kuzindua kampeni ya "Inspire to Lead!" kuelekea 8 Machi 2025, siku ya Kimataifa ya Wanawake, yenye lengo la kupambana na dhana potofu za kijinsia na kuhamasisha usawa wa fursa kwa wanawake na wasichana.