Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum

TANZANIA YAELEZA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU ZA USAWA WA KIJINSIA.

Imewekwa: 14 Feb, 2025
TANZANIA YAELEZA MAFANIKIO YA UTEKELEZAJI WA PROGRAMU ZA USAWA WA KIJINSIA.

Na WMJJWM - Marekani

Tanzania imeonesha dhamira thabiti ya utekelezaji wa kanuni zilizoainishwa katika Azimio la Copenhagen la Maendeleo ya Jamii, Mpango wa Kimataifa wa Utekelezaji wa tamko la Madrid wa 2002, Ajenda ya 2030 ya Maendeleo Endelevu, na Malengo ya Maendeleo ya Milenia.

Serikali ya Tanzania inatambua Usawa wa Jinsia na Uwezeshaji wa Wanawake ni nguzo muhimu katika kuleta maendeleo yenye tija na endelevu kwa jamii.

Hayo yamebainishwa na Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia Maendeleo ya Jamii na Makundi Maalum Wizara ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Amon Mpanju katika kikao cha 63 cha Tume ya Maendeleo ya Jamii kinachofanyika nchini Marekani kilichoanza tarehe 10 na kitahitimishwa tarehe 14 Februari, 2025 nchini Marekani.

Pamoja na hayo katika kikao hicho Serikali ya Tanzania imesema inaendelea kushughulikia changamoto za kijamii kwa kuhamashisha ushiriki wa makundi yote katika shughuli za kiuchumi na maendeleo ya kifamilia, kijamii na kitaifa.

Akiyataja baaadhi ya maeneo yaliyopewa kipaumbele Mpanju amesema maeneo hayo ni jinsia na ushirikishwaji wa jamii kwa kutekeleza sera na sheria zinazolenga kukuza uwezeshaji wa Wanawake kiuchumi kupitia upatikanaji wa ujuzi wa ujasiriamali, fursa za biashara, soko, mitaji na usimamizi wa fedha.

“Sera hizo ni pamoja na Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Jinsia ya toleo la 2023), Sera ya Maendeleo ya Biashara Ndogo na za Kati ya mwaka 2003 (SME) na Sera ya Taifa ya Kilimo 2013 na Sera ya Elimu na Mafunzo ya 2014 (toleo la 2023). Serikali imewezesha mitaji kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu baada ya marekebisho ya Sheria ya Fedha ya Mamlaka za Serikali za Mitaa Sura ya 290” amesema Mpanju.

Mpanju amesema eneo lingine ni kukabiliana na ukatili wa kijinsia, ambapo Mkakati unaolenga kukomesha ukatili dhidi ya wanawake na watoto kupitia kampeni za kitaifa za kujenga uelewa kwa jamii juu ya kupiga vita aina zote za ukatili wa kijinsia kupitia kampeni kama vile; "Twende Pamoja, Ukatili Tanzania sasa Basi), na "Siku 16 za Kupinga Vitendo vya Ukatili" unaofanyika kila mwaka kuanzia tarehe 25 Novemba hadi 10 Desemba.