TANZANIA IMEPIGA HATUA KATIKA MALEZI NA ELIMU YA AWALI KWA WATOTO: WAKILI MPANJU

TANZANIA IMEPIGA HATUA KATIKA MALEZI NA ELIMU YA AWALI KWA WATOTO: WAKILI MPANJU
Na WMJJWM-Dar Es Salaam
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Wakili Amon Mpanju amesema Tanzania imepiga hatua kubwa na muhimu za Kisera katika Malezi na Elimu ya Awali kwa Watoto Wadogo ikiwemo uzinduzi wa Program Jumuishi ya Taifa ya Malezi, Makuzi na Maendeleo ya Awali ya Mtoto ya mwaka 2021.
Wakili Mpanju ameyasema hayo tarehe 9 Septemba, 2025 mkoani Dar Es Salaam wakati akifungua Warsha ya Wadau ya Kuimarisha Mbinu Jumuishi katika Malezi na Elimu ya Awali kwa Watoto Wadogo (ECCE) nchini Tanzania.
Wakili Mpanju amesema ili kutengeneza Tanzania yenye uchumi shindani, yenye nguvu inayoweza kushindana kimataifa na kutumia fursa za kimataifa kwenye majukwaa mbalimbali ni lazima Jamii na Wadau kuungana na Serikali katika kutekeleza DIRA 2050 kwa kuwekeza kwenye sekta ya elimu hususani malezi na elimu ya awali ili hatimaye tuweze kuchangia kwenye maendeleo ya Jamii na Taifa kwa ujumla.
Amesema pia Serikali katika Dira ya Maendeleo ya Tanzania 2050 imesisitiza juu ya Elimu bora, ikiwemo elimu ya ufundi na mafunzo ya ufundi stadi kuwa ni muhimu kwa kuandaa rasilimali watu wenye maarifa, fikra bunifu na ujuzi katika maisha.
"Serikali imehakikisha shule zote za msingi zilizopo hapa nchini 20,386 zinakuwa na madarasa ya awali ambapo mpaka sasa tunayo madarasa ya awali 20,316 kwenye hizo shule. Hii ni hatua kubwa katika kutekeleza malengo endelevu na Mipango ya kitaifa." amesisitiza Wakili Mpanju
Wakili Mpanju amelishukuru Shirika la UNESCO pamoja na Hilton Foundation kwa kuandaa Mradi wa Strengthening Holistic Approaches and Practices (SHAPE) unaolenga kuhimiza utekelezwaji na Azimio la Tashkent la 2022 lililolenga kuimarisha Malezi na Elimu ya Awali kwa Watoto Wadogo sambamba na juhudi za kimataifa za kufanikisha lengo la Maendeleo Endelevu yaani (SDG) 4.2, linalozitaka nchi zote kuhakikisha kuwa kila mtoto wa kike na wa kiume wanapata huduma bora za Malezi, Maendeleo na elimu ya awali ifikapo mwaka 2030.
"Kwa msingi huo kupitia Nyenzo ya SHAPE INITIATIVE, ambayo imetengenezwa na UNESCO nyie washiriki maoni mikakati ya kuishirikisha Jamii, taasisi za Dini, Mashirika yasiyo ya kiserikali, Sekta binafsi na Wadau wa Maendeleo ili kuongeza ujenzi wa vituo hivyo nchini ambavyo ni muhimu sana kwa Ustawi na Maendeleo ya watoto wadogo." amesema Wakili Mpanju
Aidha ameeleza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imetoa maelekezo kwa Wakurugenzi wa halmashauri zote nchini kuhakikisha wanawatumia Maafisa Maendeleo ya Jamii na Maafisa Ustawi wa Jamii kuhamasisha ujenzi wa vituo vya Kulelea Watoto Wadogo mchana kila Kijiji ikiwa ni utekelezaji wa Sera za Taifa na makubaliano ya Kimataifa.
"Katika kuhakikisha Ajenda hii inatekelezwa Serikali imejumisha malezi na elimu ya awali ya watoto wadogo (ECCE) katika Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano wa 2021/22 hadi 2025/26 pamoja na kukamilisha aina kadhaa za ramani za Vituo vya Watoto wadogo mchana na imepanga kwa mwaka huu Bajeti kujenga vituo vya Watoto wadogo mchana vya kijamii (ECD) 154 kwenye Mikoa 10." ameeleza Wakili Mpanju
Vile vile amefafanua kuwa Serikali na Wadau wanaendelea na jitihada za ujenzi wa Vituo vya Watoto wadogo mchana ambapo mpaka sasa kuna takriban ya Vituo 4,636 nchini ukilinganisha na idadi halisi ya watoto ambapo kwa mujibu wa sensa ya Taifa ya 2022 Watoto wa miaka 0-4 ni 15% ya watanzania wote.
Kwa upande wake Mtaalam wa Masuala ya Elimu kutoka UNESCO nchini Tanzania Dkt. Faith Shayo, ameishukuru Serikali kwa kupiga hatua kubwa katika suala la malezi na elimu ya awali kwa watoto wadogo ikiwa na lengo la kuhakikisha kila mtoto wa kitanzania anapata elimu iliyo bora ya awali kwani ndiyo msingi wa malezi na jamii yenye maendeleo.
Warsha hiyo ya siku nne ina lengo kubadilishana uzoefu katika Malezi na Elimu ya Awali kwa Watoto Wadogo ili kuendana vyema na mahitaji ya watoto wa sasa na wa baadaye inajumuisha washiriki mbalimbali kutoka wizara za kisekta za Tanzania Bara na Zanzibar, wawakilishi kutoka Mashirika Yasiyo ya Kiserikali, sekta binafsi pamoja na wadau mbalimbali wanaohusika katika masuala ya malezi.
MWISHO