Habari

Imewekwa: Aug, 09 2022

‚ÄčSERIKALI YA SAMIA YAMALIZA SINTOFAHAMU ENEO LA MACHINGA JIJINI MBEYA

News Images

SERIKALI YA SAMIA YAMALIZA SINTOFAHAMU ENEO LA MACHINGA JIJINI MBEYA.

Na Atley Kuni, WMJJWM, MBEYA.

Serikali inayoongozwa na Mhe. Samia Suluhu Hassan imemaliza sintofahamu ya eneo la Wamachinga lililopo eneo la Uwanja wa Ndege. Taarifa hiyo imepokelewa kwenye ziara ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum Dkt Dorothy Gwajima akiambatana na Uongozi wa Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mkoa na Halmashauri ya Jiji la Mbeya ambapo, aliongea na Uongozi wa Shirikisho la Machinga ngazi ya Taifa na Mkoa huo wa Mbeya.

Waziri Dkt. Gwajima, amefika kwenye eneo hilo mapema Agosti, 09, 2022, mara baada ya kupokea taarifa ya SHIUMA kuwa wanataka kusikia Hatma ya eneo hilo ambalo likirasmishwa kwao litawasaidia kutumia fursa zilizopo kupanga maendeleo ya haraka ya kwenda pamoja na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan.

"Ndugu zangu nimefika hapa nikiwa Waziri mwenye Dhamana na Maendeleo ya Jamii Jinsia Wanawake na Makundi Maalum, ambayo ni pamoja na Machinga na hii ni kufuatia jana mliponieleza juu ya changamoto ya urasmishaji eneo hili kwamba utaratibu ukamilike haraka. Hivyo, nikaona ni vema nifike eneo la tukio nijionee mwenyewe badala ya kuambiwa alisema Dkt. Gwajima. na kuongeza "nadhani mmemsikia Kaimu Mkurugenzi, amesema eneo hili tangu mlipopewa na Mhe. Rais limeendelea kuwa la kwenu na hakuna mabadiliko yoyote.

Awali Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Mbeya Triphonia Kisiga alielezea Mbele ya Waziri Dkt Gwajima kuwa, eneo hilo lilitolewa kwa maelekezo ya Mhe. Rais, hivyo hakuna mtu ambaye anaweza kutengua maamuzi hayo labda Mhe. Rais Mwenyewe hivyo akawataka wafanya biashara hao kufanya shughuli zao kwa kujiamini.

Katika Ziara hiyo, Waziri Dkt.Dorothy Gwajima alipokea changamoto za wafanyabiashara hao ikiwepo kutokuwepo kwa Vyoo vyakutosha kwenye eneo hilo, pamoja na kutokuwepo eneo rafiki kwa wauzaji wa Maziwa wa eneo hilo.

Waziri Dkt. Gwajima, akiwa na Uongozi wa Mkoa na Halmashauri wameahidi kuchukua hatua za haraka na za dharura wakati wanapofikiria kupata suluhu ya kudumu ya uboreshaji wa miundombinu hiyo.

Katika ziara hiyo, Wamachinga kupitia Mwenyekiti wao wa Taifa, Ernest Matondo wameishukuru Serikali kwa namna wanavyowajali huku wakiwasilisha ombi la kutaka Bil. 45 zilizotengwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2022/23 kwa ajili ya kundi hilo zitumike kama Bondi kwa Benki ya NMB ili waweze kujengewa Vibanda vya Machinga kwa Nchi nzima.

Katikati ya Kikao hicho, Mwakilishi wa Benki ya NMB, Manyilizu Masanja aliwasihi Wafanyabiashara hao kuchangamkia fursa ya Mikopo inayotolewa na Benki hiyo ikiwepo Mkopo Machinga ambao Riba yake ni asilimia 14.

Waziri Dkt. Gwajima akiwa na Wataalam wa Wizara hiyo, Ofisi ya Rais-TAMISEMI wapo Ziara ya kukagua shughuli za Maendeleo na Ustawi wa Jamii katika Mkoa huo.