Habari

Imewekwa: Jun, 17 2022

SERIKALI, WADAU WAFANIKISHA MIONGOZO KWA WATOTO, YAZINDULIWA SIKU YA MTOTO WA AFRIKA.

News Images

Serikali kupitia Wizara ya maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa ushirikiano na wadau mbalimbali wa Maendeleo nchini imefanikisha kuandaliwa kwa Miongozo ya Mabaraza ya Watoto na uanzishwaji wa Madawati ya Watoto katika Shule za Msingi na Sekondari na kuizinduliwa Siku ya Mtoto wa Afrika ikiwa ni hatua muhimu katika kukabiliana na kadhia ya ukatili kwa kundi hilo ndani ya jamii.

Akizungumza katika Siku ya Mtoto wa Afrika jijini Dodoma Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima alisema kuzinduliwa kwa miongozo hiyo ni hatua muhimu katika kusukuma ajenda ya kupinga ukatili hususan kwa kundi hilo la watoto.

“Watoto nchini wamekuwa wakipitia ukatili mbalimbali ikiwemo wa mitandaoni, hivyo Serikali kwa kuliona hilo tumeshirikiana na wadau na tumefanikiwa kuandaa miongozo kwa Wanafunzi, Walimu pamoja na Wazazi ili iwe msaada katika malezi na makuzi ya watoto wetu” alisema Dkt. Gwajima.

Dkt. Gwajima ameongeza kuwa, Serikali kupitia Sera ya Maendeleo ya Mtoto ya mwaka 2008 inatambua Haki tano (5) za Msingi za Mtoto ambazo ni Haki ya Kuishi, Kulindwa, Kuendelezwa, Kushiriki na haki ya Kutobaguliwa hivyo kuzinduliwa kwa mongozo ni chachu ya kuongeza mapambano ya kumlinda Mtoto.

Dkt. Gwajima amefafanua kuwa, Miongozo hiyo itapelekwa kwenye Shule za Msingi na Sekondari pamoja na Vyuo vya kati, kwenye Madawati ya ulinzi wa Mtoto na Mabaraza ya Watoto ambayo yanakwenda kuanzishwa nchi nzima ili iwe ni fursa kwa watoto kujadiliana na kueleza madhila yanayowasibu.

Katika hatua nyingine Dkt. Gwajima, amewaomba wazazi na walezi kote nchini kuwaruhusu watoto kujiunga na kushiriki katika mabaraza ya Watoto ili kutoa fursa kwa wao wenyewe kubainisha changamoto zinazowakabili.

Akizungumza kabla ya kuzinduliwa kwa Miongozo hiyo, Mwakilishi wa Shirika la Haki Elimu Dkt. Ellen Otaru, alisema wanafurahishwa na hatua ya sasa inayochukuliwa na Serikali katika kusimamia na kuheshimu haki za Binadamu ikiwepo kuwapatia Elimu Watoto ambao walikumbwa na madhila na kushindwa kuendelea na Shule kutokana na Gharama kwa kuweka Utaratibu wa Elimu Bure.

Akitoa Maelezo ya Awali kabla ya kuzinduliwa kwa Miongozo hiyo, Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Mtoto Wizarani, Sebastian Kitiku, alisema Serikali pamoja na Wadau baada ya tafiti zake waliona umefika wakati kwa watoto kupatiwa Miongozo itakayowasaidia uendeshaji wa Mabaraza yao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, Mhe. Stanslaus Nyongo, alisema wanampongeza Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuanzisha wizara hiyo, hivyo akaahidi kushirikiana na Wizara kuhakikisha ajenda ya Ulinzi wa Mtoto inapewa kiapaumbele katika nyanja zote.

Chimbuko la Siku ya Mtoto wa Afrika ni azimio la Umoja wa nchi za Afrika (OAU) la mwaka 1991 lililokuwa na lengo la kuwaenzi Watoto kutoka shule mbalimbali za nchini Afrika Kusini hususani Kitongoji cha Soweto waliouawa kinyama na Polisi wa Serikali ya Makaburu tarehe 16 Juni,1976. Watoto hao wanaokadiriwa kufikia 2000 waliuawa wakati wanaandamana kupinga elimu ya kibaguzi dhidi ya watoto wenye asili ya kizungu.