SERIKALI KUENDELEA KUKUZA USAWA WA KIJINSIA NCHINI KUPITIA SERA, BAJETI NA MIONGOZO MBALIMBALI

Na WMJJWM - DODOMA
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Felister Mdemu, akimwakilisha Katibu Mkuu Dkt. John Jingu, amefungua kikao kazi cha kikundi kazi cha kitaifa cha kuhuisha masuala ya jinsia katika sera za kitaifa, kilichofanyika tarehe 27 Juni 2025 jijini Dodoma. Katika hotuba yake, aliwashukuru wadau wote kwa mchango wao katika kuendeleza usawa wa kijinsia, huku akisisitiza kuwa kila taasisi inapaswa kujumuisha masuala ya kijinsia katika mipango na bajeti zake.
Ameeleza kuwa Serikali imeandaa Mwongozo wa Uzingatiaji na Utekelezaji wa Masuala ya Usawa wa Kijinsia, ambao utazisaidia Wizara, Serikali za Mitaa, taasisi binafsi na asasi za kiraia kuweka sera na mipango madhubuti yenye mrengo wa kijinsia.
Katika hotuba yake, Mdemu aliagiza taasisi zote kuanzisha Dawati la Jinsia litakalosimamia utekelezaji wa ajenda za kijinsia, na kuhakikisha kuwa mipango, tathmini na miradi inazingatia tofauti na mahitaji ya kijinsia. Akisisitiza umuhimu wa hatua hizo, alisema: “Ni jukumu la kila mwajiri kuhakikisha mipango na bajeti zao zinazingatia usawa wa kijinsia ili kujenga jamii jumuishi na yenye haki kwa wote.”
Aidha, Mwakilishi wa UN Women nchini Tanzania, Usu Malya, aliipongeza Serikali kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa usawa wa kijinsia. Aliwashukuru washiriki wote kwa kujitokeza na kushiriki kikamilifu katika kikao kazi hicho. “UN Women inaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania na wadau wengine kuhakikisha kuwa ajenda ya kijinsia inaendelezwa kwa vitendo na kuleta mabadiliko ya kweli kwenye jamii,” alisema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Jinsia, Badru Abdunuru, alisema kikao kazi hicho ni sehemu ya jitihada za Serikali kuhakikisha kuwa ajenda ya jinsia haibaki kwenye maandiko bali inatekelezwa kwa vitendo katika kila sekta. “Kupitia kikao hiki, tunatarajia kuona kila taasisi ikiibua vipaumbele vya kijinsia na kuvifanyia kazi kwa ushahidi na takwimu. Lengo letu ni kuona usawa wa kijinsia unakuwa sehemu ya maamuzi, sio tu nyongeza,” alisema Badru